HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 25, 2018

MWANTIKA AANZA MAZOEZI MEPESI, YAKUBU MOHAMED KWENDA AFRIKA KUSINI KWA UCHUNGUZI ZAIDI- DAKTARI AZAM


Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii.

BEKI wa timu ya Azam Fc David Mwantika, ameanza rasmi mazoezi ya wenzake wiki hii ikiwa baada ya kuugua ghafla uwanjani wiki tatu zilizopita.

Mwantika alipata hitilafu hiyo ya mwili dakika ya 65 wakati Azam FC ikicheza hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mbagala Zakhem na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, na baadaye ya Rufaa ya Muhimbili (MNH).

Baada ya kuhamishiwa Muhimbili na kutibiwa vema kabisa, iliwalazimu madaktari wa hospitali hiyo kumhamishia kitengo cha magonjwa ya moyo cha Taasisi ya Jakaya Kikwete na kufanyiwa vipimo ili kujua kama ana tatizo la aina hiyo.

Akizungumzia hali ya mchezaji huyo, Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa tayari wamepokea majibu ya vipimo hivyo vinavyoonyesha kuwa beki huyo hana tatizo la moyo akidai yupo fiti kabisa na ndio maana wamemruhusu kuanza mazoezi mepesi.

“Mwantika alipata huduma Muhimbili na akalazwa katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete na baada ya kufanyika uchunguzi wa kina kabisa na vipimo vya kina na kuangalia mishipa ya damu ya moyo imethibitika kwamba Mwantika hana tatizo la moyo.

“Na sasa amerudi tena na katika siku mbili hizi tulianza kuangalia uwezo wake wa kukimbia na uwezo wake wa pumzi kwa hiyo alianza mazoezi ya kukimbia kwa dakika 20, dakika 30 na leo (jana) amekimbia dakika 45,” alisema.

Mwankemwa alisema kuwa wiki ijayo beki huyo ataruhusiwa kuanza mazoezi ya kawaida na wenzake tayari kabisa kurejea katika ushindani.

Akizungumzia maendeleo ya beki Yakubu Mohammed, aliyevunjika mfupa mdogo wa mguu wa kulia (fibula),  Mwankemwa alisema licha ya wiki nne kupita na kuondolewa hogo (P.O.P) bado beki huyo anasikia maumivu kwenye eneo hilo.

Daktari huyo alisema kutokana na hali hiyo, beki huyo atalazimika kwenda nchini Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi zaidi wiki hii muda wowote ili kujua tatizo linalomkabili.

“Baada ya kutolewa P.O.P imeonekana bado ule mguu una maumivu makali sana kwa hiyo uongozi uliamua kwamba aende naye akafanyiwe uchunguzi Afrika Kusini kwa hiyo  tutafanya taratibu za kutafuta Visa na Yakubu kama sio siku ya Jumatano ijayo au Alhamisi atakwenda kwa ajili ya matibabu Afrika Kusini,” aliongeza Mwankemwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad