Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kupandikizia figo wagonjwa wa nne ikiwa ni mara ya pili kutoa matibabu hayo ya ubingwa wa juu nchini.
Upasuaji huo umefanywa na wataalam wa Muhimbili kwa kushirikiana na wataalam kutoka Hospitali ya BLK ya nchini India na umekua na mafanikio makubwa kwani wagonjwa wote hali zao zinaendelea vizuri .
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Profesa Lawrence Museru amesema Novemba mwaka jana Muhimbili iliweka historia kwa kufanya upasuaji mkubwa na wa kwanza nchini kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano za kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Akifafanua amesema upasuaji huo wa figo ukifanyika nchini unagharimu Shilingi Milioni 21 na endapo mgonjwa akipelekwa nchini India matibabu yake yanagharimu Shilingi Milioni 80 hadi Shilingi milioni 100.
“Shughuli hii inatuonyesha kwamba hospitali sasa inaweza kupandikiza figo na lengo letu ni kuhakikisha huduma hii inakua endelevu ili kuokoa fedha za serikali kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi na pia kuwafikia Watanzania wengi ambao wanahitaji kupandikizwa figo,’’amesema Profesa Museru.
Amesema Hospitali ya Muhimbili itaendelea na shughuli hiyo na kwamba kila mwezi itapandikiza figo kwa wagonjwa watano hivyo kwa mwaka itafanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 60.
‘’Mipango endelevu ni kuwa na sehemu maalum ya upandikizaji figo na hivi karibuni MNH itaanza ujenzi wa jengo jipya la kulipia hivyo katika jengo hilo tutatenga sehemu maalum ya upandikizaji figo,’’ amesema Profesa Museru.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za figo kutoka hospitali ya BLK Dk.Prakash Sunil amesema ndoto yake ni kuona huduma ya upandikizaji figo Muhimbili inakua endelevu na yenye mafanikio.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk.Onesmo Kisanga amewataka Watanzania kuzingatia ulaji unaofaa na kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na presha ambayo yanachangia kuleta magonjwa ya figo.Kwa mujibu wa Dk. Kisanga nchini Tanzania kuna wagonjwa 800 ambao wapo katika huduma ya kusafisha damu.
Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya BLK ya India wakimpandikiza figo mgonjwa baada ya ndugu yake kutoa figo. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Upasuaji wa Muhimbili, Dkt. Isaack Mlatie na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Upasuaji wa Hospitali ya BLK, Dkt. Ankur Arya. Kulia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Upasuaji wa Hospitali ya BLK India, Dkt. H. S. Bhatyal wakiendelea na upandikizaji figo kwa mgonjwa.
Wataalamu wakiaandaa figo baada ya kuitoa kwa mchangiaji kabla ya kuipandikiza kwa mgonjwa.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Upasuaji wa Hospitali ya BLK India, Dkt. H. S. Bhatyal (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wengine baada ya kutoa figo kwa mchangiaji.
Kushoto ni wataalamu wakiendelea kumpatia mchangiaji huduma ya upasuaji baada ya kutoa figo wakati kulia ni figo ikiwa imeifadhiwa kwenye chombo maalumu kabla ya mgonjwa kupandikizwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari baada ya hospitali hiyo kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa wanne. Upandikizaji huo umeanza tarehe 16-04-2018 na umemalizika leo kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya BLK nchini India. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Onesmo Kisanga na Mkurugenzi wa Magonjwa ya Figo wa BLK ya India, Dkt. Sunil Prakash, Mtaalamu wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Rajesh Kumar Pande wa Hospitali ya BLK ya India na Mratibu wa Hospitali ya BLK, Manju Sharma.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo leo ambao umefanyika katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Magonjwa ya Figo wa BLK ya India, Dkt. Sunil Prakash akizungumza na waandishi wa habari leo. Kutoka kushoto ni Prof. Museru, Dkt. Rajesh Kumar Pande na Mratibu wa Hospitali ya BLK, Manju Sharma.
Wakurugenzi wa Muhimbili na wafanyakazi wengine wakifuatilia mkutano huo leo.
No comments:
Post a Comment