HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 6, 2018

BODI YA PAMBA YAONGEZA CHUPA MILIONI NNE ZA DAWA ZA KUUA WADUDU KATIKA PAMBA

Na Tiganya Vincent
Serikali kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB) imeongeza dawa zaidi za kukabiliana na wadudu waharibifu wa zao la pamba zenye thamani ya bilioni 16 ili kuwasaidia wakulima waweze kuokoa mazao yao shambani.

Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini Igunga na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania(TCB) Marco Mtunga wakati wa kampeni ya kutoa elimu juu ya unyunyuziaji sahihi wa dawa za kuua wadudu katika pamba.

Alisema dawa hizo zitarajiwa kusambazwa kwa wakulima kuanzia wiki hii ili kuwawezesha kuoka pamba yao na hatimaye waweze kupata mavuno mengi yatakayowapatia mapato mengi.

Mtunga alisema  jumla ya chupa za dawa milioni 4 zitasambazwa katika maeneo yote yanayolima pamba haba nchini.

Alisema chupa hizo ni nyongeza katika chupa milioni 2.5 ambazo tayari zimemeshasambazwa kwa wakulima wa maeneo mbalimbali yanayolima pamba hapa nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwataka wakulima wa pamba kuhakikisha wanazingatia ushauri wote ambao wataalamu kilimo na viongozi wanaowapa juu ya upigaji dawa ili mazao yao yawe na vitumba(matunda) vingi hasa kuanzia 20 na kuendelea ambavyo ndiyo vitawawezesha kupata kilo 1000 na kuendelea katika ekari moja.

Alisema wakiruhusu vitumba vingi vishambuliwe na wadudu na kudondoka chini kuna uwezekano mkubwa wa kupata mavuno hafifu na kuwafanya washindwe kupiga hatua katika maendeleo yao.

Mwanri alisema kuwa mavuno mazuri yatategemea wingi wa vitumba na ndio yatawawezesha kupata ziada itakayowapa fedha za ziada kwa ajili ya  maendeleo yatakayowaondoa katika umaskini.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa soko la pamba kwa msimu huu linatarajiwa kuzinduliwa Mei Mosi katika Wilaya ya Igunga.

Aliwataka wakulima katika miezi miwili iliyobaki kuhakikisha wanatumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha ili kutunza kwa usahihi.
  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa elimu kwa wakulima wa pamba juu ya unyunyuziaji sahihi wa dawa za wadudu waharibifu wa zao hilo  mjini Igunga.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Igunga wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akiendesha kampeni matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu katika zao la pamba jana. Picha na Tiganya Vincent

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad