Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ameunda
kamati ya watu kumi na moja watakaopitia Katiba ya kusimamia mchezo wa
ngumi za kulipwa hapa nchini pamoja na kukusanya maoni namna bora ya
kuendesha mchezo huo itakayoanza kazi kuanzia Januari 03 hadi 31
ambapo itakuwa chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) .
Akizungumza
na wadau wa mchezo huo Jijini Dar es Salaam Mhe.Waziri ameiagiza Kamati
hiyo kufanya kazi kwa pamoja katika kuunda mfumo mpya utakaolinda
maslahi ya mabondia na wahusika wote wa mchezo huo ili kuleta heshima ya
mchezo huo hapa nchini.
“Naomba
mshirikiane katika kazi hii vunjeni makundi yenu ili mfanye kazi kwa
maslahi ya Taifa na wanamasumbwi wetu,mkifanya hivyo tutaleta hamasa
kubwa kwa watu wengi kujiunga na mchezo huu ambao unaleta ajira kwa
vijana wetu”.Alisema Mhe.Waziri Mwakyembe.
Kamati
hiyo itaongozwa na mwenyekiti Emmanueli Salehe ambaye ni mdau mkubwa wa
ngumi hapa nchini,akisaidiwa na makamu Mwenyekiti Joe Enea ambaye ni
Mwalimu wa ngumi pamoja na katibu Bw.Yahya Pori ambae pia ni mdau wa
mchezo huo.
Wajumbe
katika kamati hiyo ni Bw. Habibu A.Nyogoli mwanamasumbi wa zamani,
Shomari Kimbau ambae ni muandaaji wa mapambano ya ngumi,Bw.Fike Wilson
mwalimu wa ngumi,Bw.Anthony Ruta,mdau wa ngumi,Dkt.Killaga M.Killaga
ambaye ni daktari wa wanamasumbwi hapa nchini.Wengine ni wanamasumbwi
ambao ni Bw.Ally B Champion, Bw.Rashidi Matumla,na Bw.Karama Nyilawila
ambao wameitangaza vyema nchi yetu katika mchezo huo.
Ameongeza
kuwa katik kipindi hiki cha mpito shughuli za kutoa vibali kwa
mapambano ya ndani na kwa mabondia wanaosafiri nje ya nchi zitaendelea
kutekelezwa na BMTambapo ameiagiza BMT kuendelea kusimamia vibali vya
safari za nje za mabondia kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za nchi.
Kwa
upande wake Katibu wa Baraza la Michezo (BMT) Bw.Mohamed Kiganja
ameihakikishia kamati hiyo ushirikiano wa kutosha ili kutimiza adhma ya
Serikali kuendeleza mchezo huo hapa nchini pamoja na kuwanufaisha
wanamichezo hao.
Naye
Bondia wa zamani Bw.Yassin Ustadh ameishukuru Serikali kwa kuamua
kuunda Kamati hiyo ambapo amesema itaondoa migogoro mingi na ya muda
mrefu iliyopo katika mchezo huo inayosababisha kupoteza hadhi yake na
kutowanufaisha mabondia.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza leo Jijini Dar es Salaam na Wadau wa mchezo wa ngumi hapa nchini ambapo ameunda Kamati ya Watu kumi na moja watakaoandaa Katiba ya mchezo huo ndani ya mwezi huu.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Bw. Yusuph Singo(aliyesimama) akizungumza leo Jijini Dar es Salaam na Wadau wa mchezo wa ngumi hapa nchini kabla ya Mhe Waziri Mwakyembe wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuuunda Kamati ya Watu kumi na moja watakaoandaa Katiba ya mchezo huo ndani ya mwezi huu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Mohamedi Kiganja akitoa muongozo wa kikao baina ya Mhe.Waziri Harrison Mwakyembe (aliyekaa katikati) na wadau wa ngumi nchini leo Jijini Dar es Salaam.
Mwanamasumbwi wa zamani Bw.Yassin Ustadhi akichangia mawazo wakati wa kikao cha Mhe. Waziri Mwakyembe wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na wadau wa mchezo wa ngumi leo Jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja
No comments:
Post a Comment