Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akipata maelezo ya hali
ya sekta ya mifugo na Uvuvi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali Denis
Mwila (mwenye suti nyeusi) alipotembelea kituo cha mpakani cha Mutukula leo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akipokea maelezo ya
changamoto za ukaguzi mazao ya mifugo na Uvuvi kutoka kwa Afisa Uhamiaji
Konstabo, Rahabu Joel alipotembelea kituo cha mpakani cha Mutukula leo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akiangalia mabondo ya
samaki aina ya Sangara yaliyokamatwa katika kituo cha mpaka cha Mutukula
mkoani Kagera. Kulia ni kaimu Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya Uvuvi
Mwanaidi Mlolwa katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Missenyi Limbe
Maurice. Kilo120 zilikamatwa katika kituo hicho.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akifungua mlango wa gari lililokamatwa
na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara likiwa limepakia samaki kilo
2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato zenye thamani ya shillingi
20,850,000/= kwenye mpaka wa Mlusagamba wilayani Ngara tarehe 03/12/2017.
Na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Joelson Mpina ya Halmashauri ya Wilaya ya
Ngara kuhakikisha inafufua mara moja mnada wa Mlusagamba ifikapo mwezi
Februari mwaka huu ili kudhibiti zaidi ya milioni mia moja zinazopotea kwa
wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali ya kusafirisha mifugo nje ya
nchi kwa kupita njia za panya.
Waziri Mpina aliyasema haya leo alipokutana na uongozi wa Halmashauri hiyo
pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara katika kituo cha
mpaka cha Rusumo baina ya Tanzania na Rwanda kukagua shughuli mbalimbali za
sekta za Mifugo na Uvuvi baada ya kutokea katika kituo cha Mutukula mkoani
Kagera ambapo pia alifanya ukaguzi kama huo na kukamata kilo 120 za mabondo
ya samaki aina ya Sangara yaliyokuwa yakitokea nchi jirani ya Uganda bila kufuata
utaratibu.
“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya sekta ya mifugo na uvuvi naelekeza
kwamba ifikapo Februari mwaka huu nataka miundo mbinu yote iwe
imeboreshwa na mnada wa Mlusagambo uwe unafanya kazi katika kiwango cha
mnada wa upili na mimi mwenyewe nitahakikisha ninakuja kuuzindua”lisisitiza
Mpina
Waziri Mpina alisema kutokuwepo kwa Mnada wa Mlusagambo kunaipotezea
Serikali mapato makubwa ambapo mifugo mingi imekuwa ikiuzwa katika nchi
jirani na Serikali kuambulia kiasi kidogo cha fedha kutokana na wafanyabiashara
kupita njia za panja na kufanikiwa kukwepa kulipa kodi malimbali za Serikali.
Alisema taarifa inaonyesha kuna idadi kubwa ya Ng’ombe wanaopita njia za
panya ambao hawatozwi ushuru wa kushafirishwa jambo ambalo amelilalamikia
kuwa ni hujuma na kuendekeza rushwa baina ya watendaji wa Serikali.
Aidha amesema Wizara inakusudia kuomba Serikali kupandisha ushuru wa
kusafirisha mifugo (movement permit) kufikia shilingi 50,000/= badala ya shilingi
20,000/= ya sasa kwa kuwa hailingani na hali halisi ya soko na gharama za
utunzaji wa mifugo hiyo.
“Tutahakikisha tunaiomba serikali ibadili ushuru huu kwa kuwa mfugaji anatumia
gharama kubwa za kumfuga na kumnenepesha mfugo kwa zaidi ya miaka mitano
halafu anakuja kupata shilingi 20000 tu ni jambo lisilokubalika” alisisitiza Mpina
Aliongeza kwamba baada ya kukamilika kwa mnada huo Serikali itaweka vizuizi
katika njia zote za panya ambapo pia alisisitiza watendaji wa Serikali na wananchi
kwa ujumla kuwa waadilifu na kuwa walinzi badala ya kutegemea viongozi wa
kitaifa wa Serikali kulinda utoroshaji wa raslimali za taifa ikiwa ni pamoja na
mifugo, samaki na mazao mbalimbali yatokanayo na sekta hizo.
Aidha alisema katika njia zote za panya inashangaza kuona kuna wenyeviti wa
vijiji, watendaji wa vijiji, kata, vyombo vyote vya serikali vya ulinzi na usalama pia
kuna Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya lakini utoroshaji unaendelea bila wahalifu
hao kukamatwa, ambapo aliwataka watendaji wote kuwa waaminifu na
kumwagiza Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua za mara moja watendaji
watakaobainika kujihusisha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na rushwa.
Akitolea mfano wa jinsi alivyokamata kilo 65,600 za samaki wachanga aina ya
Sangara waliokaushwa kwa chumvi wenye thamani ya shilingi milioni mia tatu
katika Kisiwa cha Lubili wilayani Muleba kwenye Mkoa wa Kagera baada ya
wamiliki wa samaki hao kukimbia hivi karibuni, alisema zoezi hilo lilifanikiwa
baada ya yeye kupata taarifa kutoka kwa raia mwema ambapo aliagiza mamlaka
za Wilaya ya Muleba kufuatilia kwa karibu hatimaye kuwakuta samaki hao
wakiwa wameanikwa chini katika kisiwa hicho.
“Naomba kusema raia mwema huyo alitoa taarifa siyo kwa sababu alilipwa fedha
bali alikuwa na uchungu na uzalendo wa dhati kwa taifa lake baada ya kuona
kwamba raslimali ya taifa inatoweka” alihoji Waziri Mpina
Aidha, Waziri Mpina alisema Wizara inapambana kuhakikisha kwamba kunakuwa
na kodi ya mifugo ambapo kila mfugo utatakiwa kulipiwa kodi tofauti na mfumo
wa sasa ambapo hakuna kodi ya moja kwa moja inayotozwa kwa mifugo.
Alisema uanzishwaji wa kodi ya mifugo utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya
mifugo katika kipindi kifupi kijacho kwa kuwa fedha itakayokusanywa itatumika
katika kununua madawa ya ruzuku kwa mifugo, chanjo, kuboresha malisho na
miundombinu mbalimbali ya mifugo ikiwa ni pamoja na majosho na malambo ya
kunyweshea maji mifugo hiyo.
Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya mifugo yote nchini
inateketea nchini wakati wa jua kali kipindi cha kiangazi kwa sababu ya kukosa
maji na malisho bora jambo ambalo ni hasara kubwa kwa taifa.
Mbunge wa jimbo la Ngara, mheshimiwa,Alex Raphael Gashaza alipendekeza
wafugaji kutambuliwa kwa kulipa kodi ya mifugo na kuanzisha vitalu maalumu vya
ranchi za mifugo ili kuthibiti magonjwa na kuinua ubora wa mifugo.
Alisema utaratibu huo pia utapunguza migogoro mingi inayojitokeza sasa baina ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ambapo ambapo pia ameipongeza
Serikali kwa juhudi inazofanya katika zoezi linaloendelea la kupiga chapa mifugo.
Akitoa ufafanuzi Waziri Mpina alisema Serikali inaruhusu uanzishwaji wa ranchi
ndiyo maana suala hilo limezingatiwa katika sheria mbali mbali za tasnia ya
mifugo ikiwa ni pamoja na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo
Namba 12 ya Mwaka 2010, Sheria ya Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo
Namba 13 ya Mwaka 2010, na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo namba 4 ya
Mwaka 2012.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele
alimweleza Waziri kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba mwaka
2017 jumla ya kilo 903,018 za mazao ya uvuvi kutoka katika maeneo ya
Mwanza,Mganza,Kagera, Kigoma na Dar es Salaam yenye thamani ya shilingi
bilioni mbili yalikaguliwa na kuhakikiwa na kuruhusiwa kusafirishwa kupitia kituo
cha mpakani cha Rusumo.
Aidha alisema kituo cha Rusumo katika kipindi hicho kimekusanya shilingi
7,058,300 kama mrahaba kwa mazao ya uvuvi yanayokwenda nje ya nchi.
Akiwa katika ziara hiyo Waziri Mpina alipata fursa ya kuliona na kukagua gari
lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter lililokamatwa na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara likiwa limepakia samaki kilo 2,000
aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato zenye thamani ya shillingi
20,850,000/= kwenye mpaka wa Mlusagamba wilayani Ngara tarehe 03/12/2017
saa tatu asubuhi ambapo aliwaelekeza watendaji kuhakikisha taratibu zote za
kisheria zinafuatwa ili kuweza kulitaifisha gari hilo kulingana na Sheria ya Uvuvi
namba 22 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 na marekebisho
yake ya mwaka 2012 na 2015.
Katika tukio hilo Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani
katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma na dereva wa gari hilo Ayoub
Sanga walishikiliwa na polisi ambapo Ngoma alisimamishwa kazi mara moja
kupisha uchunguzi.
Aidha Mshauri wa Uvuvi wa Mkuu wa Mkoa, Efrazi Mkama na maafisa Uvuvi wa
Halmashauri ya Muleba Wilfred Tibendelana na Maengo Nchimani na Afisa Uvuvi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba vijijini Renus Ruhuzi wanaendelea kuripoti
katika kituo cha polisi Bukoba kwa mahojiano ya kisheria juu ya utoroshwaji wa
samaki hao.
No comments:
Post a Comment