Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) imeendelea na Usajili wananchi Vitambulisho vya Taifa mkoani
Mtwara ambapo katika Wilaya ya Mtwara Idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza
kushiriki zoezi hilo huku baadhi wakilalamikia kukaa muda mrefu kwenye vituo
vya Usajili na baadhi ya mashine kutokufanya kazi.
Bwana Athumani Salum mkazi
wa Kata ya Magomeni amesema “zoezi kama zoezi ni zuri ila changamoto kubwa ni
kukatika kwa umeme na hivyo kusababisha wananchi tusubiri muda mrefu kiasi cha
kukatisha tamaa. Kwakuwa hili ni zoezi la kiserikali kwanini Serikali
isisaidie umeme kutokatwa kwenye vituo? ”
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Bi Rose Mdami ambaye alikuwepo kituoni hapo ameeleza changamoto ya
umeme ni kubwa katika vituo vingi vya usajili hata hivyo kwa kushirikiana na
uongozi wa Wilaya wameshachukua hatua za
kutafuta magenereta ili kazi ziendelee kama kawaida.
“ si kweli kwamba mashine
zote hazifanyi kazi katika mashine tulizonazo zipo baadhi ambazo zinatunza
umeme muda mrefu na kwahizi ambazo hazifanyi kazi kwa kukosa umeme tunaendelea
kuharakisha kupata magenereta ili kuamsha mashine ambazo zimeshindwa kufanya
kazi ili wananchi wasisubiri muda mrefu” alisisitiza
Katika kituo cha Magomeni
kilichopo shule ya Msingi Lilungu wananchi pia wamekutwa wakihangaika kutafuta
fomu zao za usajili walizosajiliwa mwaka 2014 ambapo zoezi hilo lilifanyika kwa
mara ya kwanza kwa hatua ya kujaza fomu tu
bila kupigwa picha.
Akifafanua kuhusu
wananchi hao Bi. Rose amesema kwa wale wananchi wanaofika
kwenye vituo vya Usajili na ambao walisajiliwa mwaka 2014 na kujaza fomu za
maombi ya Vitambulisho vya Taifa, pindi wanapofika
kwenye vituo vya Usajili wanachukuliwa alama za kibaiolojia, picha na saini ya
kielektroniki na kisha kuruhusiwa kuondoka kwakuwa taarifa zao msingi tayari zilishaingizwa
kwenye mfumo tofauti na wale ambao ndio kwanza wanaanza Usajili.
Mkoa wa Mtwara unakusudiwa
kusajili wananchi zaidi ya 800,000 kwa Wilaya za Mtwara, Tandahimba, Nanyumbu,
Masasi na Newala. Usajili ambao unakusudiwa kumalizika mapema mwezi Machi, 2018
na kuwezesha wananchi katika mkoa huo kuanza kutumia Vitambulisho
vitakavyozalishwa katika shughuli
mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na uzalishaji mali.
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Chiputaputa Bw. Juma Hamisi Chambeya akiwagongea muhuri wakazi wa
eneo lake kwenye fomu za maombi ya Vitambulisho kuthibitisha makazi ya wananchi
hao wakati wa zoezi la kuwasajili Vitambulisho vya Taifa likiendelea. Kabla ya
wananchi kugongewa muhuri wa Serikali ya Mtaa wananchi kwanza wanatakiwa kujaza
fomu ya maombi yenye vipengele 72 na kutoa nakala ya viambatisho vyao msingi
vinavyowatambulisha kabla fomu hiyo haijapitiwa kugongwa muhuri wa Serikali ya
Mtaa/Kijiji anakoishi.
Bi. Sharifa Said akiwa na Bi. Zubeda Abdallah ( katikati) na Bi.Rahma Ally (kulia) wakijaza fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa katika kituo cha Usajili kilichopo Shule ya Msingi Lilungu mkoani Mtwara, wakati zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu lenye kulenga utoaji wa Vitambulisho vya Taifa likiendelea Wilaya ya Mtwara.
Bi.
Asha Bakari (kushoto) na Bi. Asha Yasini (mwenye mtoto) wakazi wa Kata ya Mbaya
Mashariki wakitafuta fomu zao walizojaza mwaka 2014 waliposhiriki zoezi la uandikishaji
Vitambulisho vya Taifa; ili
wakakamilishe hatua ya mwisho ambayo ni kuchukuliwa alama za kibaiolojia, Picha
na Saini ya Kielektroniki.
baadhi
ya wananchi wa Mbaya Mashariki wakisubiri kujaziwa fomu za maombi ya
Vitambulisho vya Taifa ili wakapigwe picha, kuchukuliwa alama za kibaiolojia na
saini ya kielektroniki wakati zoezi la Usajili likiendelea kwenye Kata yao.
Wakitoa huduma hiyo ni Bi. Moza Mohamedi Lukwekwe (kulia) Mwenyekiti wa Mtaa wa
Mbaya na Bi. Asia Abdallah Nachuma (kushoto) ambaye ni mjumbe wa Mtaa wa Mbaya.
Huduma hiyo ya kuwajazia wananchi fomu za maombi ya Vitambulisho imekuwa
ikitolewa kwa wananchi wote wanaofika kwenye vituo kusajiliwa na hawajui kusoma
na kuandika ili kurahisisha zoezi.
No comments:
Post a Comment