Serikali imesaini mikataba minne na kampuni nne za ujenzi wa barabara
yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 702 kwa ujenzi wa kilomita 402.
Tukio hilo la kusaini mikataba hiyo limeshuhudiwa na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mwakilishi Mkazi wa
Benki ya Mandeleo ya Afrika (AfDB), MarieHellen Minja, wabunge ambao
miradi hiyo ya Barabara itapita majimboni mwao, Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) na wakandarasi walioshinda zabuni.
Akizungumzia utiaji saini huo, Waziri Mbarawa amesema fedha hizo
zitatumika katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tabora
(Usesula)- Koga hadi Mpanda yenye urefu wa kilomita 335 na kilomita 67
kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
Waziri Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hizo ni utekelezaji wa ilani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ahadi za Rais John Pombe Magufuli
wakati wa kampeni.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)Bi. MarieHellen Minja, wakishuhudia tukio la utiaji saini wa mikataba minne ya mradi wa ujenzi wa barabara za Tabora – Koga- Mpanda na Mbinga – Mbaba Bay (kilomita 402) lililofanyika leo jijini Dar es salaam.
Aidha, Waziri Mbarawa ametumia nafasi hiyo kuwataka wakandarasi
walioshinda zabuni kujenga barabara zenye ubora na viwango kwa
kuzingatia muda wa ujenzi.
Profesa Mbarawa ameongeza kuwa nia ya Serikali ni kuona ujenzi wa
barabara hiyo unakamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
"Naomba TANROADS msimamie ujenzi wa barabara yenye ubora kwani
wakandarasi wengi ni wajanja na ikitokea mtu ameharibu asipewe nafasi
kabisa ya ujenzi wa barabara hapa nchini," amesema Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick
Mfugale, amesema kuwa wakandarasi waliopewa kazi wametokana na
uchambuzi mkubwa uliofanyika kati ya wakandarasi 129 waliojitokeza
mwaka 2016 kuomba zabuni za ujenzi wa barabara hizo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini, Mhandisi Patrick Mfugale, akibadilishana nyaraka za mkataba mara baada ya kusaini na Mkandarasi wa Kampuni ya Jiangxi Geo Bw. Chen Xianghua leo jijini Dar es salaam, atakayejenga barabara ya Usesula hadi Komanga km 108.
Mhandisi Mfugale amefafanua kuwa ili kurahisisha ujenzi wa barabara hizo
wamegawa kwa wakandarasi wanne ambapo barabara ya Usesula hadi
Komanga kilomita 108 itajengwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering
Group Corporation Limited ya China kwa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni
158 na itajengwa kwa miezi 36.
"Komanga hadi Kasinde kilomita 108 itajengwa na Mkandarasi Kampuni ya
China Wu Yi Co. Limited kwa zaidi ya sh.billioni 140 na Kasinde hadi
Mpanda kilomita 105 Mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh
Group Co.Ltd kwa sh. Bilioni 133," amesema Mhandisi Mfugale.
Mhandisi Mfugale ameongeza kuwa barabara ya Mbinga hadi Mbamba
Bay kilomita 67 inajengwa na Mkandarasi China Henan International
Corporation Group Co.Ltd (Chico) kwa sh. Bilioni 129.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akipokea zawadi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kama ishara ya shukrani kwa ajili ya ujenzi wa barabara jimboni kwake, mara baada ya kushuhudia tukio la utiaji saini mikataba minne ya mradi wa ujenzi wa barabara za Tabora – Koga- Mpanda na Mbinga – Mbaba Bay (kilomita 402) lililofanyika leo jijini Dar es salaam.
Amesema TANROADS imejipanga kusimamia ujenzi huo kwa kufuata
viwango vinavyohitajika vya ujenzi wa barabara nchini.
Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Bi. Minja amesema ofisi yake itaendelea kutoa
mchango kwa serikali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini pale
watakapo hitajika.
Bi. Minja amesema kuwa matarajio ya AfDB ni kuona Tanzania inapata
maendeleo kwa haraka na njia rahisi ni kupitia miundombinu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye barabara
ya Tabora hadi Mpanda inapita jimboni kwake ambapo amesema kuwa
ujenzi huo utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya,
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
amesema barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania,
Msumbiji na Malawi. Amesema kuwa Nyasa ina vivutio vingi vya utalii hivyo ujio wa barabara
hizo utakuwa njia rahisi ya kuwafikisha watalii eneo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye pia ni
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, akimkabidhi zawadi
Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Bi. MarieHellen Minja, mara baada ya
kushuhudia tukio la utiaji saini wa mikataba minne ya mradi wa ujenzi
wa barabara za Tabora – Koga- Mpanda na Mbinga – Mbaba Bay zenye
jumla ya (kilomita 402), jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment