Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu (kati kati), akiwatoa hofu Watendaji wa
Mamalaka ya Vitambulisho vya TAifa (NIDA) kwamba kuanzia mwezi January 2018, Idara ya Uhamiaji
Zanzbar imejipanga kushughulikia maombi ya Vitambulisho vya Taifa kwa Raia wote watakaofika
katika Ofisi yao iliyopo Kinduni, Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, badala ya kufuata huduma Ofisi ya
Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini iliyopo Kivunge. Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ahadi za Serikali kufikisha
huduma karibu na Wananchi. Aliyasema hayo wakati alipotembelea Ofisi hizo wakati wa ziara ya
kikazi katika Wilayani humo tarehe 05 - 06 Disemba, 2017.
Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, amewapongeza
watendaji wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa kusogeza huduma za
Uhamiaji karibu na Jamii inayowazunguka. Alitoa pongezi hizo leo alipotembelea Vituo
Maalum “Detached Points” vilivyopo ndani ya maeneo ya Kendwa na Nungwi, Shehia za
Nungwi - Banda Kuu, Mnarani na Kiungani, Wilaya ya Kaskazini “A” na Fukwe za
Kiwengwa, Pongwe na Pwani mchangani, Shehia za Kiwengwa, Moga na Pongwe kwa
Wilaya ya Kaskazini “B” alipofanya ziara ya kikazi katika Wilayani hizo tarehe 05 – 06
Disemba, 2017.
Mkoa wa Kaskazini Unguja ni kitovu cha shughuli za Biashara na Uwekezaji katika sekta
ya Utalii, hali inayosababisha kuwavuta wageni wengi kutoka Mataifa mbali mbali
Duniani kutembelea maeneo hayo kwa madhumuni tofauti. “katika Mkoa huu Idara yetu
ina kazi kubwa ya kuhudumia wageni wanaoingia na kuishi ndani ya Mkoa huu, kwani ni
Mkoa ambao huwavuta wageni wanaokuja kutembea na kupumzika kwenye fukwe
nadhifu, kuna wanaokuja kwa kuwekeza na wale wanaokuja kufanyakazi na biashara
mbali mbali za Utalii, hali ambayo huibua changamoto nyingi za Kiuhamiaji” alisema
Kamishna Sururu.
Kutokana na muingiliano huo wa wageni wa makundi tofauti, Idara ya Uhamiaji yenye
dhamana ya kuhakikisha wageni wote wanaoingia na kuishi nchini wanafanya hivyo kwa
mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Uhamiaji, ina mchango mkubwa katika
kuimarisha Ulinzi, Uchumi na Utamaduni wa watu wa Zanzibar. Kuanzishwa kwa Vituo
maalum kwenye maeneo hayo ni mapinduzi makubwa katika Udhibiti na Usimamizi wa
wageni wanaoingia na kuishi Zanzibar kinyume cha Sheria.
“Kwa kweli Nimefarijika sana kuona jinsi mlivyojipanga kuweza kuyafikia maeneo yote
yenye changamoto za uwepo wa baadhi ya wageni wanaojipenyeza na kuishi nchini bila
ya Kufuata Sheria za Uhamiaji. Uwepo wa Vituo hivi naamini ni muarobaini wa kuondoa
kabisa tatizo la Uhamiaji haramu” Alisema Kamishna Sururu na kuongeza “Hatuzuwii
wageni kuja kutembea, hatuzuwii wageni kufanyakazi ama kuwekeza nchini kwetu bali
tunataka wageni wote waingie na kuishi nchini kwa kuheshimu Sheria za Nchi yetu, kwa
kufanya hivyo tutaweza kufikia ile adhma njema ya serikali kufungua milango ya
Biashara na Uwekezaji katika sekta ya Utalii kwa manufaa makubwa bila ya kuathiri
Jamii na Tamaduni zetu”.
Aidha, Kamishna Sururu aliwahakikishia Masheha wa maeneo hayo kuwa Idara ya
Uhamiaji itaendelea kushirikiana nao kwa vitendo hususan katika kupiga vita Uhalifu wa
aina zote ukiwemo Udhalilishaji, Uuzaji na Usafirishaji wa Madawa ya Kulevya
unaofanywa na baadhi ya wageni hapa Zanzibar.
Kufuatia kauli hiyo, Sheha wa Shehia ya Nungwi - Banda Kuu, Bw. Mohamed Khamis
Haji alisema “Nashukuru sana kwa ujio wako na hasa msimamo ulioutoa juu ya
kuwachukulia hatua stahiki wageni wanaojihusisha na vitendo vya Uhalifu hapa Nungwi.
Hichi ni kilio chetu cha siku nyingi. Nasi tunaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano
unaostahiki kwa Askari wa Uhamiaji ili Shehia zetu ziendelee kupokea wageni wenye
manufaa kwa Jamii zetu na si vinginevyo”.
Kwa upande wake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mrakibu Mwandamizi wa
Uhamiaji, Muhsin A. Abdullah alifafanua, lengo kubwa la kuanzisha kwa vituo hivyo
maalum vilivyopo maeneo ya Nungwi na Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini “A” na“B” ni
mkakati mmojawapo katika kuimarisha Doria na Misako ili kuwabaini wahamiaji
wasiofata sheria.
“Mkoa huu tumekuwa tukilalamikiwa sana kwamba wageni wengi huzagaa na
kufanyakazi kiholela hususan kutoka Mataifa ya Afrika Mashariki, kumepelekea tusogee
karibu tuweze kushirikiana na watendaji wenzetu wakiwemo Masheha na Wananchi,
hatua ambayo imeanza kuzaa matunda. Tumeongeza wigo wa kuelimishana, kujenga
mashirikiano na kupeana taarifa mbali mbali ambazo husaidia sana utekelezaji wa
majukumu yetu” alisema Mrakibu Mwandamizi Muhsin.
Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Kiwengwa Bw. Maulid Masoud Ame katika ziara
hiyo aliapata fursa ya kuchangia ambapo alisema “Idara ya Uhamiaji inatusaidia sana
katika suala zima la kuwatambua nani Raia wa Tanzania na nani mgeni. Maana katika
maeneo yetu tuna changamoto kubwa sana ya kuwepo kwa vitendo vya ukiukwaji wa
maadili na udhalilishaji vinavyofanywa na watu mbali mbali wakiwemo wageni.
Hivyo
kwa ushirikiano mkubwa tunaopata kutoka kwa Askari wa Uhamiaji unatusaidia sana
kufikia maamuzi. Tumekuwa tukipokea malalamiko hayo kwa mfano yakihusisha jamii
za Kimasai wanaofanyakazi katika mahoteli mbalimbali hapa Kiwengwa, ambao baadhi
yao ni wamasai kutoka Kenya, ambapo sisi tunaona hao wote ni Watanzania wenzetu.
Askari wa Uhamiaji kwa utaalamu na weledi walionao hutusaidia katika kuwatambua”
alisisitiza Sheha Ame.
Akihitimisha ziara yake kwenye Wilaya mbili hizo, Kamishna Sururu, alitembelea Bandari
ya Mkokotoni kujionea changamoto mbali mbali zikiwemo, vipenyo vinavyotumiwa na
wahamiaji wasiotaka kufuata Sheria na uwepo wa baadhi ya Manahodha wa vyombo
vya usafiri wanaotumia Bandari hiyo, kutoshusha Abiria kwenye eneo lililotengwa.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Askari wa Uhamiaji Wilayani humo, kusimamia
vyema majukumu yao kwa mujibu ya Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. “Nawasihi na
kuwataka muelewe kuwa sisi tumepewa dhamana na Serikali kuwatumikia wananchi,
hivyo nidhamu na heshima ya kazi ndio msingi wa mafanikio katika utekelezaji wa
majukumu yetu”. Alimalizia Kamishna Sururu.
No comments:
Post a Comment