

UTATA umeighubika familia ya Jackson Makundi ambayo kijana wake aliyetambulika kwa jina la Humphrey Makundi,Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo kupotea katika mazingira tatanishi.
Utata wa kupotea kwa mwanafunzi huyo unatiliwa shaka zaidi na familia hiyo baada ya kufukuliwa kwa kaburi ulimozikwa mwili uliookotwa mto Ghona mita 300 ,jirani na shule hiyo ukidaiwa kushabihiana na wa mwanafunzi huyo
Humphrey Makundi, mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scolastica anatajwa kupotea tangu Novemba 7 mwaka huu akiwa shuleni hapo huku wanafunzi wenzake wakiendelea na mitihani ya kidato cha Pili ya upimaji ya kitaifa .
Familia ya kijana huyo yenye makazi yake mkoani Dodoma ikalazimika kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa za kupotea kwake ikidai mazingira ya kutoweka kwake ni ya kutatanisha na baadae kuwasilisha taarifa katika kituo cha Polisi cha Himo .
Kutokana na kuwepo kwa taarifa za kuokotwa kwa mwili huo ,familia iliwasilisha maombi katika mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi na mahakama ikaamuru kufukuliwa kwa Kaburi hilo zoezi lililoanza majira ya saa 8:30 mchana na kudumu kwa zaidi ya saa moja.
Jeshi la Polisi liliongoza zoezi hilo katika makaburi ya Karanga huku likishuhudiwa na ndugu wa mtoto aliyepotea ambapo baada ya mwili kutolewa kaburini hali ya simanzi ilionekana katika nyuso za baadhi ya ndugu wa Mwanafunzi huyo akiwemo baba mzazi wa kijana huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro,Kamishna Msaidizi wa Polisi ,Hamis Issa akathibitisha uwepo wa tukio hilo huku akieleza kuwa tayari jeshi la Polisi linawashikilia wati 11 akiwemo mmiliki wa shule hiyo Edward Shayo huku likifanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo mawili.
Mwili uliofukuliwa katika makaburi ya Karanga upande wa marehemu wasiokuwa na ndugu ulipelekewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC kwa uchunguzi zaidi chini ya uangalizi wa jeshi la Polisi wakishirikiana na madaktari kutoka KCMC.










No comments:
Post a Comment