
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini, Abdul-Razaq Badru (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Wateja wa Wakubwa Benki ya CRDB, Goodluck Nkini wakiangalia namna Mfumo huo mpya wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu namna unavyofanya kazi wakati wakionyesha moja ya vifaa vinavyotumika kufanikisha mfumo huo, kilichokuwa kikionyeshwa na Meneja Biashara wa tawi la Benki ya CRDB Azikiwe, George Yatera. Wakati wa uzinduzi wa Mfumo huo uliofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam, Novemba 15, 2017.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) pamoja na
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini, Abdul-Razaq
Badru (wa pili kushoto) wakipata maelezo juu ya Mfumo mpya wa utoaji
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka kwa Meneja Biashara wa tawi
la Benki ya CRDB Azikiwe, George Yatera. Wakati wa uzinduzi wa Mfumo huo
uliofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es
Salaam, Novemba 15, 2017.
Benki ya CRDB na Bodi ya Mikopo
elimu ya juu leo wamezindua utekelezaji wa mfumo mpya wa utoaji mikopo kwa
wanafunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha “IFM”. Akizungumza katika
uzinduzi huo uliofanyika katika Chuo hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB
Dokta Charles Kimei alisema mfumo huo mpya umesaidia kuongeza kasi na ufanisi
wa utoaji mikopo kwa wanafunzi kwani sasa hivi mkopo unapatikana ndani ya
dakika 15 tu tokea kuanza kujisajili.
“Mfumo huu unakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu kwa kuongeza kasi na ufanisi ambao utasaidia kuondoa
changamoto ambazo zilikuwa zikijitokeza hapo awali”alisema Dokta Kimei.
Dokta Kimei alisema mfumo huo mpya wa utoaji mIkopo unatokana na juhudi za
Benki ya CRDB, Bodi ya Mikopo na Taasisi za Vyuo Vikuu nchini kufanikisha
kuunganisha mifumo yao ya mawasiliano na utoaji huduma hivyo kurahisisha
upatikanaji wa taarifa muhimu kwa ajili ya utoaji mikopo, jambo litakalosaidia
kupunguza mzigo kwa maafisa mikopo na hivyo kuongeza kasi na ufanisi.
“Mfumo
huu ni madhubuti kwani umetengenezwa kwa kushirikisha wadau wakuu na hivyo
kuzingatia changamoto za mfumo wa awali”, alisema Dokta Kimei.
Akielezea juu ya mfumo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Tanzania
(HESLB) Abdul-Razaq Badru alisema mfumo huo utasaidia upatikanaji wa mikopo
kwa wanafunzi kwa wakati na hivyo kutoa fursa kwa wanafunzi kujikita katika
masomo badala ya kutumia muda mwingi kufuatilia mkopo yao. “Tunajua hapo awali
ilikuwa inachukua wiki mbili hadi tatu kwa mwanafunzi kuingiziwa mkopo kwenye
akaunti yake, jambo ambalo lilikuwa linaleta usumbufu kwa wanafunzi na hivyo
kujikuta wakipoteza muda mwingi katika ufuatiliaji.
Dokta Kimei ametueleza hapa
sasa hivi ndani ya dakika 15 mkopo unakuwa umeingia kwenye akaunti ya
mwanafunzi, tunajivunia sana kwa maboresho haya makubwa”, alisema Ndugu
Badru.
Bwana Badru pia aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika
kuisaidia bodi hiyo ya mikopo kwa elimu ya juu nchini katika kuboresha utendaji
wake akibainisha kuwa mfumo huo pia utasaidia katika utunzaji wa taarifa za
wanafunzi hivyo kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa urejeshwaji wa mikopo pindi
mwanafunzi anatakapo maliza masomo yake.
“Uunganishwaji wa mfumo huu na mifumo ya vyuo vikuu itatusaida kupata taarifa za
wanafunzi kwa urahisi na hivyo kuondoa changamoto za utoaji wa mikopo kwa
mwanafunzi mmoja mara mbili, mkopo kwenda chuo tofauti na alichosajiliwa
mwanafunzi pamoja na kutusaidia katika kipindi cha urejeshwaji wa mikopo” alisema
Bwana Badru.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Kitengo cha Taaluma na
Utafiti Dkt.Imanueli Mnzava Aliishukuru Bodi ya Mikopo na Benki ya CRDB kwa
kukichagua chuo hicho katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mfumo huo
mpya wa utoaji mikopo kwani wanafunzi wengi wa chuo hicho wameanza kunufaika
na utekelezaji huo. “kwa kiasi kikubwa mfumo umesaidia kupunguza changamoto
ambazo maafisa mikopo wa chuo walikuwa wakikumbana nazo kwani wanafunzi
sasa hivi wanapata mikopo kwa wakati kitu ambacho kimetusaidia hata sisi kujikita
katika ufundishaji zaidi”, alisema Dkt. Mnzava.
Akihitimisha hafla hiyo fupi ya uzinduziwa mfumo huo, Dokta Kimei aliushukuru
uongozi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa kukubali kuanza utekelezaji
wa mfumo huo, huku akisema Benki hiyo imeanza usambazaji wa vifaa vya usajili
kwa vyuo vingine nchi kwa ajili ya awamu ya pili. “Tunafaraha kuona zoezi hili
linaenda vizuri, baada ya kukamilisha hapa awamu ya pili itakuwa kwa Chuo Kikuu
Dar es Salaam, UDOM, Mzumbe pamoja SUA”, alisema Dkt. Kimei.
Katika uzinduzi huo wadau pia walipata fursa ya kuona namna mfumo huo ukifanya
kazi ambapo wanafunzi wengi walijitokeza huku wengi wakiipongeza Bodi ya
Mikopo na Benki ya CRDB kwa kubuni mfumo huo ambao umewasaidia kupata
mikopo kwa wakati.
No comments:
Post a Comment