Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Timu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 Serengeti Boys wameendelea limbwi la ushindi baada ya jana kutoka kifua mbele kwa kuifunga Cameroon katika mchezo wa kirafiki uliofanyika nchini Cameroon.
Timu hizo zitarudiana tena katika mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kesho Jumatano, Mei 3, mwaka huu.
Mbali na hilo, Afisa habari wa Shirikisho Alfred Lucas amesema kuwa timu ya Serengeti Boys imebadilishiwa kituo kutoka Port Gentil na sasa imepangiwa Libreville.
Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Niger, Angola na Mali ambako watafungua nayo mchezo Mei 15, mwaka huu. Kwa mabadiliko hayo, Kundi A lenye timu za Cameroon, Ghana, Guinea pamoja na wenyeji Gabon, litakuwa Port Gentil.
Kwa sasa Serengeti Boys wako Cameroon kwa kambi ya wiki moja iliyoanza Aprili 29, mwaka huu ambako tayari imecheza na wenyeji Cameroon mchezo mmoja na kushinda bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Yauonde.
Timu ya Serengeti inahitaji kushinda mechi mbili za mwanzo ili kujihakikishia nafasi ya kwenda kombe dunia la vijana chini ya miaka 17 litakalofanyika nchini India.
No comments:
Post a Comment