Mmoja
wa wanafunzi katika Kituo cha Jemolojia Arusha, Zuwena Mtoo, akionesha
utaalam wa kukata na kung’arisha madini ya Vito, baada ya kupata mafunzo
katika Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
Imeelezwa kuwa jumla ya wanawake 47 wamehitimu mafunzo ya ukataji
na ung’arishaji wa madini ya vito yanayotolewa na Kituo cha Jemolojia jijini
Arusha ambacho kipo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
Hayo yalisemwa jijini Arusha na Kaimu Mratibu wa Kituo hicho, Erick
Mpesa wakati wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite
unaofanyika jijini Arusha katika Kituo hicho.
Mpesa alisema kuwa mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2014
ambapo katika Awamu ya kwanza wanafunzi 15 walihitimu, Awamu ya Pili
walihitimu wanafunzi 14 na Awamu ya Tatu walihitimu wanafunzi 18.
Mkufunzi Msaidizi katika Kituo cha Jemolojia Arusha, (TGC), Lilian Petro (wa kwanza kulia) akionyesha madini ya vito yaliyong’arishwa na wanafunzi wanaopata mafunzo katika Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito (TANSORT), Archard Kalugendo, wa Pili kushoto ni Mhe. Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na wa kwanza kushoto ni Beatrice Lupi, Mhasibu Mkuu kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
“Mafunzo haya hutolewa kwa muda wa miezi Saba ambapo Wanafunzi
hawa ambao huwa na umri wa chini ya miaka 30 wanafadhiliwa na Mfuko
wa Kuwaendeleza Wanawake chini ya Kamati ya Maonesho ya Vito ya
Arusha (AGF) na Wizara ya Nishati na Madini,” alisema Mpesa.
Mratibu wa TGC aliongeza kuwa Kituo hicho pia kinaendesha shughuli za
uchongaji wa mawe ya miamba kwa kutengeneza vinyago vyenye maumbo
mbalimbali kama ya wanyama, ndege, samaki na vitu mbalimbali vya
urembo.
Akizungumzia mafanikio ya kituo hicho, Mpesa alisema kuwa mbali ya
kusaidia wanawake hao kupata mafunzo yatakayowasaida kujiajiri au
kuajiriwa, Kituo hicho ni cha pekee Afrika Mashariki kinachoendeleza
taaluma ya uongezaji thamani madini ya vito na miamba.
Samadu Mohamed, kutoka Kituo cha Jemolojia Arusha, akionesha moja ya vinyago
vinavyotokana na mawe ya miamba vinavyotengenezwa katika kituo hicho.
Kuhusu mipango ya kuendeleza Chuo hicho alisema kuwa, Chuo
kimepanga kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya diploma ambapo
mitaala ya kozi mbalimbali za taaluma ya vito na usonara imeandaliwa na
kuwasilishwa katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambapo
mchakato wa ithibati na usajili unaendelea.
Kwa upande wake Mkufunzi Msaidizi wa TGC, Lilian Petro, alisema kuwa
mafunzo hayo husaidia wanafunzi hao kutambua madini ya aina
mbalimbali, kuyakata na kufahamu thamani ya madini husika.
Aidha Lilian, Alitoa ushauri kwa wanawake mbalimbali nchini kujiunga
katika fani hiyo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito kwa kuwa
inamsaidia mtu kujiajiri kwa kuanzisha vituo vya ung’arishaji wa madini ya
vito ndani ya nchi na pia kuajiriwa.
No comments:
Post a Comment