Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Stephen Magoiga akifungua rasmi mafunzo kwa wadau wa TASAF kwa vijiji vitatu katika Kata ya Mwakipoya ili kuwajengea uelewa katika kuwaudumia walengwa.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya Kishapu, Sospeter Nyamhanga akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga ambaye alikuwa mgeni rasmi kufungua rasmi mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga (hayupo pichani).
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Stephen Magoiga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga, Stephen Magoiga ameagiza watendaji wa vijiji kuhakikisha
wananchi waliochukua fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Taifa (TASAF) bila kuwa na
sifa wanarudisha mara moja.
Magoiga alitoa agizo hilo jana wakati akifungua mafunzo
kwa wadau wa TASAF kwa vijiji vitatu katika Kata ya Mwakipoya ili kuwajengea
uelewa katika kuwaudumia walengwa.
Alisema lengo la mpango wa TASAF ni kusaidia kaya
zisizo na uwezo hivyo ni wajibu wa wadau hasa wajumbe wa Serikali za vijiji kuhakikisha
wanawatambua wananchi wa maeneo yao ili kubaini kaya maskini.
Mkurugenzi aliwataka wadau kusimamia vizuri walengwa akisisitiza
kuwa Serikali kupitia TASAF ina jukumu la kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na
maisha bora kwa kuwapa ruzuku ili kujiendeleza.
Magoiga aliongeza kwa kuwahimiza wadau hao kufuatilia
maendeleo ya watoto wa walengwa wa mpango huo wanaopata ruzuku kwani elimu
ndiyo inaweza kuondoa umaskini.
“Mpango wa TASAF ni pamoja na matumizi mazuri ya fedha na
mimi nawapongeza kwa kazi nzuri ya kuzihudumia kaya maskini, natambua kuwa
ninyi ni watu muhimu katika kushughulikia mpango huu,” alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Wilaya ya Kishapu,
Sospeter Nyamhanga alisema mafunzo hayo yataongeza ufanisi kwa wadau hao katika
kutoa huduma kwa walengwa.
Nyamhanga alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa wanabaki
na kaya maskini na zenye sifa mfuko huo ngazi ya wilaya itaendelea kufanya uhakiki
mara kwa mara kwenye vijiji lengwa.
Alisema mafunzo hayo tayari yametolewa katika vijiji 15
kati ya 78 vilivyopo kwenye mpango na kuwa lengo ni kufikia vijiji vyote ili
wadau wapate elimu ya ufanisi wa kutoa huduma.
Kwa upande wa mafanikio ya TASAF wilayani humo, alisema
kuwa hadi sasa walengwa wamepata maendeleo kupitia ruzuku wanayopokea .
Alitaja mafanikio hayo ni baadhi yao wameweza kununua
mifugo, kuanzisha biashara ndogondogo, kilimo na hata kuboresha makazi yao kwa
kuezeka kwa mabati badala ya nyasi kama ilivyokuwa awali.
Hata hivyo, alisema pamoja na hayo bado kuna changamoto
ya ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kuedeshea mafunzo kwa wadau wa mpango wa TASAF
hali inayochangia kuwa idadi chache ya mafunzo.
Tayari mafunzo hayo yametolewa kwenye vijiji vitatu
kata ya Mwakipoya na yanahusisha wadau mbalimbali wanaohudumia kaya maskini
wakiwemo watendaji kata na vijiji, mratibu elimu kata, watumishi wa afya pamoja
na walimu. Ngeme,Mwangongo na Mwakipoya.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliipongeza TASAF
na kusema kuwa yamewapa mwanga na kuwa yatawasaidia katika utendaji kazi wao.
No comments:
Post a Comment