Naibu Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kikanda,Dk Susan Kolimba
Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
Wizara ya
mambo ye nje na ushirikiano wa kikanda ametoa ufafanuzi juu ya tatizo la
watanzania waliopo Msumbiji wanaokabiliwa na changamoto ya kurudishwa nyumbani.
Akizungumza
na Waandishi wa habari mapema jijini Dar es Salaam leo Naibu Waziri wa Mambo ya
nje na ushirikiano wa kikanda, Dk Susan Kolimba amesema kuwa amepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania
waliokuwa wakiishi katika mji wa Monte Puez ulio Cabo Delgado, Jamhuri ya
Msumbiji.
Na kuweka
wazi kuwa Serikali ya Msumbiji imekiri kuwepo kwa operesheni maalum ya
kuwakamata na kuwarudisha raia wa nchi za kigeni wanaoishi katika mji huo bila
kufuata Sheria za Uhamiaji za nchi hiyo. Aidha, Serikali hiyo imetaarifu
kwamba, zoezi hilo limeanzia mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa
kigeni ikilinganishwa na miji mingine.
“ Kufuatia
hali hiyo, Ubalozi wetu nchini Msumbiji upo eneo la tukio ili kufuatilia suala
hili na kujionea hali halisi. Aidha, unaendelea kufanya mawasiliano ya Kidiplomasia
na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao. Inakadiriwa
kuwa, Watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi na kufanya shughuli za
kiuchumi na kijamii katika mji huo wa Monte Puez.
Kuanzia
zoezi hilo lilipoanza, Raia wa Tanzania wapatao 132 wamesharudishwa nchini.
Tarehe 11/02/2017 walirejeshwa raia 58. Tarehe 14/02/2017 wamerejeshwa raia 24
na leo tarehe 15/02/2017 wamesharejeshwa raia 50 ”amesema Naibu Waziri.
Ameongeza kuwa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia
Watanzania kuwa uhusiano kati ya Tanzania na jirani yetu Msumbiji ni mzuri. Hivi
karibuni mwezi wa Desemba 2016, Tanzania na Msumbiji zilifanya mkutano wa
ujirani mwema uliolenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Pemba ulio Cabo Delgado uliainisha maeneo
ya ushirikiano yakiwemo masuala ya biashara na uhamiaji.
No comments:
Post a Comment