Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amekutana na wadhibiti ubora wa shule wa halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kujua changamoto wanazokumbana nazo na mambo yanayopelekea kushuka kwa elimu katika mkoa wa Rukwa.
Zelote Stephen alifikia uamuzi wa kuwaita wadhibiti hao baada ya Mkoa wa Rukwa kushuka kielimu kutoka nafasi ya 6 mwaka 2015 hadi nafasi ya 12 kati ya Mikoa 31 kwa mwaka 2016 kwa mitihani ya kidato cha 4, na pia kuteremka katika mitihani ya kidato cha pili kutoka nafasi ya 20 kwa mwaka 2015 hadi nafasi ya 21 kwa mwaka 2016.
Wadhibiti hao walielezea sababu kede kede zilizopelekea kushuka kwa kiwango cha elimu katika Mkoa wa Rukwa na miongoni mwao ni kutopewa mrejesho wa taarifa za kila wiki wanazoziandika na kukabidhi kwa wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya.
“Toka Mwezi July mwaka jana tumeshaandika ripoti nyingi tu zinazoelezea mapungufu kama vile, upungufu wa waalimu kwa baadhi ya masomo, matundu cha vyoo, vitabu vya kusomea, nakadhalika lakini hakuna hata mrejesho tunaoupata kutoka kwa Mkurugenzi,” Goreth Ntulo alieleza.
Kwa upande mwingine sababu zinazokwamisha ufanisi wa kazi za wadhibiti hao wanadai kutopewa motisha na mwajiri wao na kuwasababisha kuishi katika maisha magumu.
“Mimi sijawahi kwenda likizo kwa fedha ya serikali tangu nianze kufanya kazi na madarasha hatupandishwi n ahata ukipandishwa inabaki jina tu lakini mshahara upo pale pale na kuapata hiyo fedha ya daraja ulilopandishwa ni kazi kubwa ya kukatisha tamaa,” Mmoja wa wadhibiti hao Mama Jairo alifafanua.
Nae Mkuu wa Mkoa baada ya kusikiliza malalamiko hayo aliwaagiza wakurugenzi wote kuhakikisha kwamba wadhibiti hao wanapatiwa mrejesho juu ya kasoro walizozibaini baada ya kufanya ukaguzi katika mashule hayo.
“Kwani hizi shule ni za nani?, Si ni za wakurugenzi, sasa naagiza wakurugenzi wote wawe wanatoa mrejesho kwenu ili muweze kujua ni lipi linawezekana kurekebishika na kwa kipindi gani na nili lipi haliwezekani ili Mkae mkijua, bila ya hivyo itakuwa haina maana nyinyi kufanya ukaguzi halafu ripoti zikarundikwa kwenye madroo,” Zelote Stephen alikazia.
Pia Mkuu wa Mkoa aliwasisitiza wakati wakaguzi hao wanawapa wakurugenzi ripoti hizo wahakikishe kuwa wanawapa na “dead line” na wakurugeni wazingatie na wawaheshimu na kuwathamini ili kila mmoja afanye kazi yake ambayo ameajiriwa nayo.
“Kama Mlikuwa na uwoga muondoe ofisi hii itawapa sapote, na make mkijua kuwa tunawathamini sana maana kupitia nyinyi tunajifunza mengi sana ambayo ndio yanatupa mpango mkakati wa kuhakikisha tunapeleka elimu mbele,” Zelote Stephen aliwahakikishia.
Mmoja wa wadhibiti hao Pracida Rwegasira alitoa shukrani zake za dhati kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa kuchukua uamuzi wa kuwaita ili kutoa mchango wao katika kupeleka sekta ya elimu mbele na kuongeza kuwa tokea aanze kazi hiyo hawajawahi kuitwa na Mkuu wa Mkoa.
Nae Katibu Tawala wa Mkoa Tixon Nzunda aliahidi kutetea haki zao za kiutumishi na kuwa sauti ya kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elmu.
No comments:
Post a Comment