Katibu Mkuu wa Kamati ya Paralimpiki Tanzania Tuma Dandi akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waadishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu udhamini wa GAPCO wa mbio za kilometa 10 za Kilimanjaro Marathon. Kushoto ni Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania Caroline Kakwezi.
Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania Caroline Kakwezi akisisitiza kuwa GAPCO itaendelea kushirikiana na TPC na kuwema itagharamia usafiri, malazi na chakula kwa washiriki wote kutoka Dar es Salaam na kwa washiriki kutoka Moshi na Arusha watapewa usafiri.
Na Mwandishi wetu
Kamati ya Paralimpiki Tanzania imeipongeza GAPCO Tanzania kwa mchango wake mkubwa unaohakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika michezo hususani mbio za Kilimanjaro Marathon.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Kamati hiyo, Tuma Dandi alisema wamekuwa na ushirikiano wa miaka saba sasa na GAPCO ambayo imekuwa ikiwafadhili watu wenye ulemavu kushiriki katika mbio hizo.
“Sisi kama TPC tumeguswa mno na jitihada hizi za GAPCO kwani wamekuwa msaada mkubwa kwetu kwa muda wote huu na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika michezo. Hii ni taasisi ya kuigwa ili kupiga vita unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu,” alisema na kuongeza kuwa kuna michezo ya aina nyingi tu ambayo watu wenye ulemavu hushiriki na inahitaji udhamini.
Alisema kwa mwaka huu watafanya mchujo ili kupata wawakilishi watakaosafiri Moshi kushiriki katika Kilimanjaro Marathon. Mchujo huo utafanyika katika Uwaja wa Uhuru Jumamosi Februari 11 kuanzia saa mbili asubuhi. Arusha na Moshi pia watafanya mchujo kama huu lakini siku na tarehe tofauti na hii ya Dar es Salaam.
“Tunawaomba watu wenye ulemavu wajitokeze kwa wingi katika mchujo huu ambapo tutapata timu ya watu 37 watakaotuwakilisha kule Moshi Februari 26 katika mbio za Kilimanjaro marathon,” alisema.
Aliipongeza GAPCO kwa kuendelea kudhamini mbio za kilometa 10 kwa walemavu kwa miaka saba sasa kwani mbio hizo zimekuwa mwaka hadi mwaka.
Meneja Masoko wa GAPCO, Caroline Kakwezi alisisitiza kuwa GAPCO itaendelea kushirikiana na TPC na kuwema itagharamia usafiri, malazi na chakula kwa washiriki wote kutoka Dar es Salaam na kwa washiriki kutoka Moshi na Arusha watapewa usafiri.
Alisema GAPCO itaendelea kufanya kazi kwa karibu na kamati hiyo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaendelea kushiriki katika mbio za Kilimanjaro Marathon bila matatizo yoyote. “Tumeridhishwa na kazi wanayoifanya TPC na tuna kila sababu ya kuendelea kushirikiana nao,” alisema.
Mbio za mwaka huu zinatarajiwa kuwa kubwa zaidi kushinda mwaka jana huku usaJili ukianzia Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mlimani City Februari 18 na 19 mwaka huu.
Mbali na GAPCO wadhamini wengine wa Kilimanjaro Marathon 2017 ni, Kilimanjaro Premium Lager-42 km, Tigo 21km na Grand Malt kilometa tano. Wengine ni KK Security, TPC Limited, FNB, Kibo Palace, Kilimanjaro Water, CMC Automobile, Rwandair, Keys Hotel, Anglo Gold Ashanti na KNAUF Gypsum.
No comments:
Post a Comment