Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu Mwakyanjala akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu ulaghai kupitia simu za mkononi unaofanywa na matapeli katika kipindi hiki. Kulia ni Afisa Uhusiano wa TCRA Bi. Mabel Masasi
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) leo Jijini Dar es salaam. (Picha na Frank Mvungi-Maelezo)
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuwa
makini na utapeli unaofanywa kupitia simu za mkononi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na
Kaimu Meneja Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu
Mwakyanjala wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Semu alisema kuwa kuna ongezeko la matapeli
wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma pesa kwa simu za
mkononi hivyo Mamlaka na vyombo vya usalama vinashughulikia suala hilo.
“Usitekeleze maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa mawasiliano
ya simu hata kama yanatoka kwa mtu unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa
namba nyingine ili kuthibitisha’’ alifafanua Semu.
Alitahadharisha kuwa mtu akipokea taarifa kwa njia
ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kimakosa na kutakiwa
kuzirudisha asifanye hivyo mpaka atakapojiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.
Akizungumzia matumizi ya huduma za kifedha kwa
njia ya mitandao, Semu alibainisha kuwa kwa miezi miwili ya Novemba na Desemba
2016 jumla ya fedha iliyopita kwenye mitandao ya simu za mkononi ni shilingi
trilioni 13.07 hali inayothibitisha ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za
kifedha kwa njia ya mitandao hapa nchini.
Alitaja makampuni yaliyohusika na takwimu za
miamala hiyo kuwa ni Zantel (EASY PESA), Tigo (TigoPesa), Vodacom (M PESA),
Airtel (Airtel Money) na Halotel (HALOPESA).
Aidha aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi
kuhusu matapeli na kuwasilisha malalamiko yao ya huduma za mawasiliano kwa TCRA
kupitia sanduku la posta 474 Dar es salaam au wafike kwenye ofisi za TCRA
zilizo karibu au wapige simu namba 0784 558270, 0784 558271 na barua pepe (malalamiko@tcra.go.tz)
No comments:
Post a Comment