Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limeufungia uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuchezwa mechi za ligi kuu na daraja la kwanza hadi utakapofanyiwa marekebisho.
Uwanja huo unamilikiwa na Chama cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro umekosa vigezo vya kutumika kwenye ligi kutokana na miundo mbinu yake hasa sehemu ya kuchezea kutofaa hivyo kuanzia leo hautatumika hadi utakapofanyiwa marekebisho.
Uwanja huo hutumika kwa mechi mbili tu za ligi zinazohusisha timu za Simba na Yanga zinapocheza na Mtibwa Sugar kutokana na uwezo wake wakuingiza watu wengi kwakua miamba hiyo ya soka nchini ina mashabiki lukuki.
Mechi namba 151 (Mtibwa Sugar vs Simba). Baada ya mchezo kumalizika mashabiki waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. Pia kamera ya Azam Tv upande wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.
Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas alisema katika mchezo kati ya Mtibwa na Simba uliofanyika uwanjani hapo wiki mbili zilizopita ulikosa mvuto na kuzifanya timu hizo kushindwa kuonyesha kandanda safi kutokana na ubovu wa dimba hilo.
TFF imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia kilichangiwa na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya kusimamia usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika kutazama mechi.
Vilevile sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika hali mbaya ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
Hivyo, Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ili kutoa fursa kwa wamiliki kufanya marekebisho makubwa kwenye eneo la kuchezea (pitch), na pia askari polisi kupata maelekezo ya kutosha ya jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama mechi. Kama marekebisho hayatafanyika, uwanja huo hautatumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
No comments:
Post a Comment