HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 13, 2016

TIBA YA MOYO KUANZA KUTOLEWA KWA MADAKTARI WA MICHEZO- TFF

Ofisa habari  wa Shirikisho la Mpira wa Miguu TanzaniaTFF Alfred Lucas 

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeanza mazungumzo na Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko Muhimbili, Dar es Salaam ili kwa pamoja waanze  kushiriana kutoa mafunzo kwa madaktari na wahudumu wa afya kwa wanamichezo wa soka katika kushughulikia matatizo ya moyo.
Akizungumza leo Jijini Dar es salaam, Ofisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema kuwa mafunzo haya yataboresha uwezo wa madaktari wa mpira wa miguu sambamba na kusambazwa kwa vifaa maalumu vya tiba ya moyo kwenye klabu za soka nchini.
Lucas amesema hii ni hatua thabiti inayochukuliwa na uongozi wa TFF baada ya kutokea vifo vinavyosababishwa na mshtuko wa moyo kwa wachezaji ukiwamo ugonjwa wa ‘cardiac arrest’ ambao kwa taarifa za awali zimeonyesha ndio chanzo cha  kifo cha Mchezaji wa Mbao FC U20, Ismail Mrisho Khalfan.
Marehemu Ismail Mrisho Khalfan alifariki dunia baada ya kuanguka uwanjani Desemba 4, 2016 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera wakati timu yake ya Mbao ikicheza na Mwadui katika mechi ya ligi ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.
 Kifo hicho kimegusa hisa za wanafamilia wengi wa mpira wa miguu akiwamo Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA), Bw. Gianni Infantino ambaye juzi alituma salamu za rambirambi kwa Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Emil Malinzi kutokana na kifo cha ghafla cha Mchezaji.
Rais Infantino, ametuma salamu za rambirambi ambazo zinakwenda sambamba na za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Ndugu Nape Nnauye na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou.
Ismail aliyeanguka uwanjani dakika ya 74, alipata huduma ya kwanza uwanjani hapo kwa madaktari waliokuwa uwanjani, lakini baadaye taarifa za kitabibu zilionyesha amefariki dunia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad