Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
BAADA ya kupata udhamini wa milioni 25 kutoka kwa kampuni ya Hawaii Products Supplies kupitia bidhaa yake ya Cowbell, timu ya Mbao Fc ya Jijini Mwanza wameamua kuingia zaidi msituni kwa ajili ya kujiandaa na ligi kuu Vodacom duru la pili kwa kuvaana na Stone Sugar ya nchini Kenya.
Mbao iliyopanda daraja msimu huu, imeweza kuwa na matokeo chanya tofauti na watu walivyodhani imeingia mkataba huo leo mbele ya waandishi wa habari na baadhi ya viongozi wengine wa timu hiyo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini, Mwenyekiti wa Mbao, Solly Njashi amesema kuwa mkataba huo utawasaidia hasa katika maandalizi ya timu yao na zaidi kiwango cha fedha kinaweza kuongezeka kutokana na matokeo watakayokuwa wanayapata kwenye ligi.
Njashi amesema kuwa, hatua hii ni nzuri sana kwao na wamefurahi sana kupata udhamini huu na wanategemea kufanya vizuri zaidi kwani uwepo wa kocha wao Etien Ndailagije kumewawezesha kuwa na kikosi kipana zaidi huku malengo yake yakiwa ni kuinua zaidi vijana.
Kwa upande wa Meneja Masoko Hawaii, Erisalia Ndeta amesema kuwa wameridhishwa na na kiwango cha Mbao Fc mpaka kufikia hatua ya kuwapatia udhamini huo wa miezi sita ila wanatarajia utakuwa ni endelevu kwani wana imani wataendelea kufanya vizuri.
Ndate amesema kuwa, udhamini huo unaweza kuongezeka zaidi kulingana na kiwango cha timu kitakavyokuwa kwani huu ni mwanzo tu na wanaweza kufanya mengi zaidi.
Mbao imefanikiwa kupata udhamini huo baada ya kuweza kuonyesha kandanda safi zaidi, kwa sasa timu hiyo ipo kambini na inatarajiwa kuondoka Jumapili asubuhi kuelekea Rorya kucheza na Stone Sugar ya nchini Kenya ikiwa ni moja ya maandalizi.
Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi (kulia) akisaini mkataba wa makubaliano ya udhamini Mhasibu Mkuu wa kampuni ya Hawaii Products Supplies Said Khamis wakishuhudiwa na Meneja Masoko Hawaii, Erisalia Ndeta leo Jijini Dar es salaam. Picha ya chini wakikabidhiana mkataba huo.
Mhasibu Mkuu wa kampuni ya Hawaii Products Supplies Said Khamis akimkabihi jezi Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi (kulia) yenye nembo ya Cowbell leo Jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Mbao, Solly Njashi (wa pili kutokam kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utiaji wa saini wa mkataba wao na kampuni ya kampuni ya Hawaii Products Supplies, kulia ni Meneja Masoko Hawaii, Erisalia Ndeta, kutoka kushoto ni Meneja Mkuu Msaidizi Mohamed Saleh, na Mhasibu Mkuu wa Hawaii, Said Khamis.
Picha na Zainab Nyamka.
No comments:
Post a Comment