Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kesho kwenye kongamano la kwanza la Majasiri (Alumn) la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) litakalokuw ana kauli mbiu ya "Mafunzo na huduma za Afya nchini Tanzania, tulikotoka, tuliko sasa na baadaye".
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Makamu Mkuu wa Chuo wa MUHAS, Prof. Ephata Kaaya amesema kuwa kongamano hilo ni la kujenga umoja na jumuiya kwa wahitimu wa MUHAS na kutoa fursa kwa wahitimu ili kujenga uhusiano mzuri na chuo,Skuli, Taasisi na Kurugenzi zake.
Katika mkutano huu mada kuu zitakuwa ni mbili na zitawasilishwa na kufuatiwa na majadiliano ya kina kuhusiana na mada hizo mbali na hilo kutakuwepo na maonyesho ya ya mambo mbalimbali yahusuyo kazi za chuo, baadhi ya vifaa tiba na dawa mbalimbali.
Kaaya amesema kuwa, Desemba 02, kutakuwa na sherehe ya utoaji wa zawadi Academic Prize Giving Ceremony kwa wanafunzi wanaohitimu waliofanya vizuri katika kipindi cha masomo yao chuoni na jumlka ya wahitimu 79 watapata zawadi hizo, Kwa ngazi ya Shahada ya kwanza wahitimu 49, wanawake wakiwa 17 na wanaume 32. Jumla ya zawadi 70 zitatolwa kwa wanafunzi 39 wa shahada ya uzamili wakiwemo wanawake 15 na wanaume 24.
Mahafali ya ya 10 ya MUHAS yenye jumla ya wahitimu 944 kati ya hao 372 ni wahitimu wa kike ambao ni sawa na asilimia 39.4 yanatarajiwa kuwa Desemba 03, na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Rais Mstaafu Mh Alhaji Dk, Ali Hassan Mwinyi atawatunukia wahitimu wa ngazi ya diploma na digrii mbalimbali ambapo mwaka huu jumla ya wahitimu 376 watatunukiwa stashahada na wahitimu nane watapata stashahada za ngazi za juu katika fani mbalimbali za afya na sayansi shirikishi.
Kaaya amesema kuwa kwa mara ya kwanza MUHAS wameweza kuongeza idadi ya wahitimu wa shahada ya uzamivu na kufikia saba toka kuanzishwa mwaka 2007, Pia wahitimu 367 watapata shahada ya kwanza 183 shahada ya uzamili huku wahitimu wawili watatunukiwa digeii za uzamili za utaalamu yaani Super Speciality.
No comments:
Post a Comment