HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 10, 2016

MIILI YA WATU TISA KATIKA AJALI YA BOTI MTO RUVUMA YAPATIKANA

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Satano Mahenge, amesema kuwa kazi ya kuwatafuta watu waliozama maji katika ajali ya boti kwenye kivuko cha mto Ruvuma kutoka kijiji cha Mkenda Songea kwenda kijiji cha Mitomoni Nyasa iliyotokea Julai 02, 2016 imekamilika. Boti hiyo inayokadiliwa kubeba watu kati ya 30 hadi 50 ilipata dhoruba iliyopelekea kupinduka na kusababisha vifo vya watu tisa (9) huku wengine 36 kuokolewa.

Kazi ya kutafuta miili hiyo iliyopotea ilianza Julai 03, 2016 na kufikia tamati jana Julai 09, 2016.  

“Napenda kuwajulisha wananchi wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kuwa miili yote tisa ya watu waliozama imepatikana. Taratibu za mazishi zimefanyika kwa familia zikishirikiana na Serikali”. Alisema Dkt. Mahenge.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Satano Mahenge alipokuwa aliekekea kijiji cha Mitomoni Nyasa kuzitembelea familia zilizopoteza ndugu zao kwenye ajali ya boti Mto Ruvuma hivi karibuni.

Waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni Omari Jela (miaka 11) alipatikana Julai 05, 2016, Fadhili Hamis Fadhili (miaka 8) alipatikana Julai 05, 2016, Hadija Said (miaka 41) alipatikana Julai 06, 2016, Zulfa Ally (miaka 14) alipatikana Julai 06, 2016, Awetu Mohamed (miaka 14) alipatikana Julai 06, 2016.

Wengine ni Omar Waziri (miaka 13) alipatikana Julai 06, 2016, Stumahi Abdallah (miezi 5) alipatikana Julai 07, 2016, Rajabu Said Machupa (miaka 17) alipatikana Julai 08 ,2016 pamoja na Tupishane Mustafa (miaka 5) alipatikana tarehe 09 Julai, 2016.

Mkuu wa Mkoa amewapongeza  wale wote walioshiriki na kufanikisha zoezi la utafutaji wa miili hiyo, na kuwashukuru wananchi wa vijiji vya Mkenda na Mitomoni kwa ushirikiano wao walioutoa kwa kikosi kazi alichokiunda kusimamia zoezi la utafutaji miili. Pia  Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa kutoa boti ya kisasa iliyofanya kazi kubwa na nzuri ya kutafuta miili ndani ya mto Ruvuma.  Boti hii imesaidia sana kufanikisha kazi ya upatikanaji wa maiti ndani ya Mto Ruvuma.  

Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo kwa Wakuu wa Wilaya zote za Ruvuma, kuwa wafanye kazi ya kuvitambua na kuanisha vivuko vyote vilivyopo ndani ya maeneo yao, wafanye sensa ya vyombo vya usafiri vinavyotumika kuvusha abiria na mizigo na kuona umakini wake, wawatambue wamiliki na waendeshaji wa boti kwenye mito na Ziwa Nyasa na waweke utaratibu wa abiria wote kujisajili kila watumiapo vyombo vya majini.

Pia amewasihi wananchi wote kuzingatia Sheria na Taratibu kila watumiapo vyombo vya moto ili kuepusha ajali zinazosababisha vifo na ulemavu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad