Wamiliki wa magari makubwa (Maboza) ya kusambaza huduma ya Majisafi katika maeneo ambayo bado
haijafikiwa na huduma hiyo jijini Dar es salaam, wametakiwa kutumia magari hayo kusambaza Majisafi na
salama ili kuepukana na adha ya kuugua magonjwa ya mlipuko yakiwamo magonjwa ya kipindupindu kwa
watumiaji wa Maji hayo.
Hayo yamezungumzwa na Afisa mtendaji Mkuu wa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam
(Dawasco), Mhandisi Cyprian Luhemeja katika kikao cha pamoja na wamiliki hao wa magari ya kusambaza
huduma ya Maji kwa wananchi waishio jijini Dar es salaam na mkoa wa Pwani.
Mhandisi Luhemeja, amewataka wamiliki hao kujali afya ya wateja wao ambao ndio watumiaji wakuu wa
Maji hayo kwa kusambaza huduma ya Majisafi na salama ili kuepuka adha ya kuugua magonjwa ya
mlipuko yakiwamo magonjwa ya kipindupindu, kwani Dawasco imewaamini na kuwapa kibali cha
kusambaza Maji kwa wananchi.
“Tumieni Magari yenu kusambaza Majisafi na salama, tumewaamini tumewapa kibali cha kutoa huduma ya
Majisafi na salama kwa wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma hii, kuweni wawakilishi wazuri ili
kwa pamoja tujenge nchi yetu” alisema Luhemeja.
Aidha, Mhandisi Luhemeja ameahidi kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma hiyo, pamoja na kutatua
changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma hiyo, ili wamiliki hao waweze kutoa huduma
bora kwa wateja pamoja na wananchi wote.
Naye, mwenyekiti wa umoja huu wa wamiliki wa magari ya kusambaza huduma ya Maji Bw. Fredrick
Mayunga amepongeza juhudi zinazofanywa na Dawasco pamoja na ushirikiano mzuri uliopo baina yao na
shirika, kwani unawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kufanya kazi na kuwa wawakilishi wazuri
kwa jamii wanayoihudumia.
“Tunawashukuru sana kwa ushirikiano wenu, namna ambavyo mnatambua umuhimu na mchango wetu
katika kutoa huduma ya Maji kwa wananchi, tunaahidi kutoa huduma bora kwa jamii kwa kusambaza
Majisafi na salama kama Afisa Mtendaji mkuu alivyoagiza” alisema Mayunga.
Dawasco iliamua kushirikiana na wamiliki wa maboza kwa kuanzisha vizimba vya Maji kwenye maeneo
mbalimbali jijini Dar es salaam ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya Maji katika maeneo ambayo
hayana miundombinu ya Majisafi.
Mmoja wa wamiliki wa magari yakusambaza huduma ya maji kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na
huduma hiyo ya Maji Steven Peter akichangia kwenye kikao cha pamoja cha wamiliki wa maboza na
Dawasco kilichofanyika makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment