Mabalozi wa nchi za Afrika waliopo Kenya, jana waliadhimisha sherehe za Siku ya Afrika (AU Day), ambazo ziliahirishwa mwezi uliopita kupisha Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira kuhusu Afrika, uliofanyika Nairobi. Siku ya Afrika huadhimishwa Mei 25 kila mwaka.
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Kenya, Balozi Amina Mohamed, alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo zilizofanyika viwanja vya Ubalozi wa Malawi jijini Nairobi. Katika hotuba yake, Waziri huyo alisema nchi za Afrika simepiga hatua katika kujenga amani na utengamano chini ya Agenda 2063, inayolenga kuliinua bara hili kiuchumi.
Chini ya mpango huo, Afrika imekusudia kumaliza kabisa mizozo ya kivita na mifarakano mingine kati ya nchi wanachama ifikapo mwaka 2020. Malengo mengine makubwa ni kupunguza utegemezi nje wa bajeti ya mipango ya maendeleo ya Afrika, na kuondoa vikwazo vya miingiliano ya watu, bidhaa na huduma baina ya nchi za bara hilo.
Waziri Mohamed alisema Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na mawaziri wa Mambo ya Nje watapatiwa pasi za kusafiria za Afrika mwezi Oktoba mwaka huu chini wa mpango wa kuondoa vikwazo vya usafiri barani Afrika. Sherehe hizo ziliandaliwa na Mabalozi wa Kundi la Afrika (African Diplomatic Community) nchini Kenya, akiwemo Balozi wa Tanzania, Mhe. John Haule.

Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Kenya, Balozi Amina Mohamed (wa pili kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule, alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonyesho ya kusherehekea Siku ya Afrika. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Monica Juma na kushoto ni mke wa Balozi Haule, Bibi Maria.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Balozi Monica Juma, akitizama bidhaa za kutoka Tanzania kwenye maonyesho hayo.

Wageni kwenye banda la Tanzania.

Banda la Tanzania kwenye sherehe za Siku ya Afrika

Na sasa ni wakati wa kuserebuka! Balozi Haule (wa tatu kulia), Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Fastjet, Bw. Jimmy Kibati (wa pili kulia) na mshereheshaji, wanajimwaga uwanjani baada ya Balozi kukabidhi washindi wawili (kushoto) tiketi za kwenda Dar es Salaam na kurudi kwa ndege ya Fastjet.

No comments:
Post a Comment