Mwenyekiti wa Stand United Amani Vicent akitolea ufafanuzi suala la mgogoro uliopo sasa kwenye klabu ya Stand United
Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii.
UONGOZI wa klabu ya Stand United umesema kuwa hawawatambui wanachama wanaosajiliwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga zaidi wanataka kuja kuiharibu timu hiyo ambayo imetoka kwenye mfumo wa wanachama na kuingia kwenye kampuni huku tayari wakiwa kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni 24 mwaka huu na zaidi wamefika mbali na kutishia kwenda kuwashtaki Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Mwenyekiti wa Stand United, Amani Vicent amesema kuwa wameshawasilisha malalamiko yao Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kufuatia mchakato unaoendelea kufanywa na kamati ambayo haitambuliki inayowaandikisha wanachama wapya ikiwa wanachama halali walioanzisha Stand United walishakubaliana kwenye mkutano mkuu kuibadilisha timu hiyo kwenda kampuni na tayari wameshasajili.
"Kuna kamati ambayo imeundwa na Mkuu wa Wilaya ambayo awali ilivua uanachama wa Stand ikiwemo mimi mwenyewe ila baada ya kulifuatilia na kwenda hadi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye na kurudisha mamlaka juu yetu lakini bado wanaendelea kufanya vitu vya kihuni kwa kupita mtaani na kusambaza fomu za kujisajili uanachama,".
Amesema, wanachokifanya ni kinyume na taratibu na hata ukienda kwa msajili wa klabu utaona ni wanachama gani wanaojulikana wakati wa usajili na zaidi wametangaza hadi tarehe ya uchaguzi ambao hautambuliki ila kwa upande wetu tumeshatangaza na tunafanya Juni 24. Zaidi klabu yetu kwa sasa iko kwenye mfumo wa kampuni na kama TFF watashindwa kutolea ufafanuzi suala hili la Kamati ya mkuu wa Wilaya badi hatutakuwa na budi na kwenda mbele zaidi kupelekea malalamiko yetu FIFA na ushahidi tunao.
"TFF wanajua kama tumeshaleta malalamiko kuhusiana na mchakato unaoendelea sasa wa kusajili wanachama wapya na kama watashindwa kutolea ufafanuzi sisi tutakwenda mbele zaidi ambapo tutapeleka na ushahidi ili haki iweze kutendeka kwani katiba yetu inajionesha wazi kabisa kuwa Stand United ipo chini ya kampuni na uongozi wake unajulikana,"amesema Vicent.
Kwa sasa Stand United ipo chini ya Mkurugenzi Mkuu Mtendaji, Jonas Tiboroha pamoja na Mwenyekiti Amani Vicent na wapo kwenye hatua za mwisho za kuelekea uchaguzi mkuu na wameshawasilisha tarehe yao TFF na wana imani watashirikiana vizuri.
No comments:
Post a Comment