Programu ya uboreshaji wa miundombinu ya masoko, uongezaji thamani mazao na huduma za kifedha vijijini (MIVARF) imefanikiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi endelevu wilayani Chato kwa kuziwezesha kaya za vijiji hivyo kujiongezea kipato, kuboresha miundo mbinu ya masoko na kuongeza ya thamani ya zao la mpunga.
Programu hiyo imeweza kuwajengea uwezo wazalishaji wadogo na kuwaunganisha na masoko na Taasisi za kifedha, kutoa mafunzo ya uongezaji wa thamani wa mazao pamoja na ukarabati wa barabara za vijiji hivyo zinazoanzia mashambani pia na ukarabati wa ghala la kuhifadhi mazao na ujenzi wa soko la mchele.
Akiongea wakati timu ya ufuatiliaji na tathmini ya MIVARF ilipotembelea wilaya hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari alieleza kuwa wananchi 3,961 kutoka katika vijiji 12 vya kata tatu za Nyamirembe, Kigongo na Ichwankima tayari wamenufaika na utekelezaji wa Programu hiyo.
Baadhi ya wakazi wa wilayani chato wakifuatilia maelezo ya mtaalamu wa ufuatiliaji na Tathmini kutoka MIVARF, Wangael Wilfred (hayupo pichani) wilayani hapo wakati wa ufuatiliaji utekelezaji wa Programu hiyo katika wilaya hiyo.
“Programu hii imeweza kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 28.1 za vijijini zinazo anzia mashambani kwa gharama ya Tsh. 1,118,235,000. Kukarabatiwa kwa barabara hizi kumepunguza gharama za kusafirisha mazao kutoka mashambani na nyumbani hadi kwa wanunuzi kutoka Tsh 2,000 kwa gunia moja hadi Tsh1,000 kwa gunia moja.” Alisema Hari.
Hari alifafanua kuwa Programu hiyo imeweza kukarabati ghala la kuhifadhi mazao katika kijiji cha Nyamirembe ambapo ghala hilo litasaidia wakulima kuendesha mfumo wa stakabadhi ya mazao gharani suala ambalo litasaidia kukabiliana na kudorora kwa bei ya zao la mpunga hasa wakati wa mavuno.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi; Joel Hari akifafanua jambo kwa mtaalamu wa ufuatiliaji na Tathmini kutoka MIVARF, Wangael Wilfred alipofika ofisini kwake wakati wa ufuatiliaji utekelezaji wa Programu hiyo katika wilaya hiyo.
Mmoja wa wakulima wa zao la mpunga katika kata ya Kigongo, Ngavune John alifafanua kuwa kutokana na uwezo wa kilimo cha kisasa waliojengewa na MIVARF kupitia SIDO Kagera tayari mavuno yameongezeka kutoka gunia 5 kwa ekari moja hadi gunia 25 kwa ekari moja kwa msimu wa mwaka jana na wameunganishwa na masoko ya uhakika.
Mratibu wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima wilayani humo SIDO Kagera,… alibainisha kuwa vikundi vya uzalishaji wa mpunga wilayani humo vimeunganishwa na taasisi za kifaedha kwa ajili ya kupata mikopo ya kilimo na kujiwekea akiba.
Naye mtaalumu wa Ufuatiliaji na tathmini kutoka MIVARF, Wangael Wilfred alibainisha kuwa Programu hiyo inalenga kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wakulima wadogo wadogo, wajasiriamali wadogo wadogo vijijini na Asasi ndogondogo za kifedha zinazotoa huduma vijijini ili kuweza kufanikisha azma ya serikali ya kupunguza umasikini na kuogeza kasi ya ukuaji wa uchumi endelevu kwa kuziwezesha kaya za vijijini kujiogeza kipato na usalama wa chakula.
Sehemu ya ghala la kuhifadhi mazao liliokarabatiwa na MIVARF katika kijiji cha Nyamirembe wilayani Chato.
Sehemu ya soko la mchele linalojengwa na MIVARF katika kijiji cha Nyamirembe wilayani chato.

No comments:
Post a Comment