Mansipaa ya Temeke imetenga kiasi cha sh bilioni 1.5 kwa mwaka huu wa fedha
wa 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi, kiwango cha lami kipande cha barabara ya Mbozi chenye urefu
wa kilometa 1.3 kinachopiota nje ya Kiwanda cha Mabati cha Alluminium Africa (ALAF).
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi leo (jumapili), mkurugenzi wa manispaa ya Temeke,
Photidas Kagimbo alisema manispaa yake imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa
kipande hicho cha barabara chenye urefu wa kilometa 1.3.
Alisema ujenzi huo utafanyika baada ya malalamiko ya muda mrefu ya wafanyabiashara wa eneo
hilo wakiwemo wamiliki wa viwanda ambako barabara hiyo inapita ikiunganisha ile ya Mbozi hadi
barabara ya Nyerere, jirani na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Alisema awali walifanya mazungumzo na kiwanda cha ALAF na Steel Masters ili kuangalia jinsi
ya kutatua changamoto hiyo na baada ya ufuatiliaji wa muda mrefu hatimaye hivi sasa itajengwa
ifikapo mwaka mpya wa fedha 2016/2017.
“Ni changamoto ya muda mrefu lakini sasa imepata ufumbuzi” alisema na kuongeza kuwa awali
ilikuwa inajengwa ili iweze kupitika lakini kutokana na shehena za mizigo mizito zinazopitishwa
katika barabara hiyo uhai wake unakuwa wakati wa kiangazi na mvua zikinyesha kunakuwa na
mashimo makubwa.
Alisema magari yenye mizigo mizito ambayo mengine ni hadi tano 40 ni changamoto kwa
barabara hiyo lakini hata hivyo sasa inajengwa kiwango cha lami hivyo itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuwapunguzia adha wenye viwanda na pia wafanyabiashara wa soko la Mapambano.
Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti na mandishi wa habari hizi, wafanyabiashara katika soko
hilo la Mapambano walidai kuwa wanapata shida hususan siku za mvua kwani magari yamekuwa
hayapiti barabara hiyo zaidi ya yale ya mizigo mikubwa.
“Wateja wetu ambao wanatumia magari madogo au yale yenye uzito uziozidi tani tatu na nusu
hawawezi kutufikia na mbaya zaidi hata sisi wenyewe wakati mwingine tunashindwa kufika katika
fremu zetu” alisema Grace Sanga.
Katibu wa Jumuia ya Vikundi vya Wenyeviwanda na Biashara Ndogondogo (Vibindo), wilaya ya
Temeke Paul Luanda alikiri kuwepo kwa adha hiyo ambayo inawakwamisha kibiashara hususan
nyakati za mvua.
“Hata hivyo manispaa Temeke inatupa ushirikiano kwani hivi karibuni ilitoa mabomba kwa ajili ya
kutusaidia kuondoa maji ili magari yaweze kutufikia na sisi kufanyabiashara” alisema na
kuongeza kuwa mashimo makubwa yanafanya magari madogo kushindwa kupita eneo hilo hivyo
wao kukosa biashara.

No comments:
Post a Comment