Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (wa pili kulia) akitembea mitaani eneo
la Chake Chake Pemba, Zanzibar kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu usalama wao katika
kipindi cha uchaguzi kisiwani humo. Waziri Kitwanga ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa
Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdullah (kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba,
Omari Khamis Othman (wapili kushoto aliyevaa kaunda suti) na Katibu Tawala wa Mkoa wa
Kusini Pemba, Ahmed Khalid Abdulla (kushoto, aliyevaa tai. Kitwanga aliridhishwa na juhudi
za kuimarisha ulinzi katika kisiwa hicho.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani) mara baada ya kuuzunguka msitu wa Taifa wa Ngezi, uliopo Wilaya ya
Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar
walisambaza taarifa za uongo kuwa kuna wakimbizi wamejificha katika msitu huo baada ya
kukimbia vurugu kisiwani humo. Hata hivyo hakuna mkimbizi yeyote aliyekuwepo katika msitu
huo na wananchi wapo katika makazi yao wakiendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato.
Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman. Kulia ni Mkuu wa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nasri.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akizungumza na wauza nguo
wa Soko Kuu la mjini Chake Chake, Pemba. Wananchi hao walikuwa wanaendelea na shughuli
zao kama kawaida bila wasiwasi wowote. Waziri Kitwanga pia alisikiliza maoni ya wananchi
hao kuhusu uchaguzi mkuu na kuridhishwa na juhudi za kuimarisha ulinzi katika kisiwa hicho.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akimuuliza swali Mkazi wa Wawi,
Chake Chake Pemba, bibi Zabibu Mohamedi, wakati Waziri huyo alipokuwa anatembea mitaani
kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2016. Hata
hivyo wananchi hao walimuahkikishia kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika siku hiyo ya
uchaguzi. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akiwahoji wafanyakazi wa Bandari Kuu
ya Pemba kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2016. Wafanyakazi hao
walimuhakikishia kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na pia wananchi hao wapo salama na
wanaendelea na shughuli zao zakujipatia kipato za kila siku.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kulia) akiwauliza maswali wananchi
wa mjini Chake Chake, Pemba kuhusu jinsi walivyojiandaa na uchaguzi wa Machi 20, 2016 na
kutoa maoni yao kama kuna tatizo lolote. Hata hivyo wananchi hao walimuambia Waziri
Kitwanga wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, hakuna vitisho vyovyote katika eneo lao.
Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati) akizungumza na wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama, mjini Chake Chake, Pemba, kuhusu masuala mbalimbali ya
uimarishaji ulinzi katika kipindi cha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2016. Kushoto
meza kuu ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdullah na kulia ni Mkuu
wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Na Felix Mwagara wa MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi
wa Zanzibar waondoe hofu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu visiwani humo.
Akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na wananchi hao wakati
alipokuwa anatembelea mitaa mbalimbali ya Soko Kuu la mjini Chake Chake,
Pemba aliwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato
kama kawaida na hakuna mtu atakayewabughudhi kwani ulinzi umeimarishwa, na
waachane na uzushi wa kutokea vurugu unaoenezwa visiwani humo.
Waziri Kitwanga alianza matembezi hayo mitaani mara baada ya kufanya
mazungumzo na Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Chake Chake ambapo
walimuhakikishia kuwa, Pemba yote ni salama na ulinzi umeimarishwa na hakuna
atakaye fanyiwa vurugu kwa mtu yeyote atakayefuata sheria.
Waziri Kitwanga aliwataka wananchi hao kuondoa hofu wanapowaona askari
mbalimbali wakipita mitaani kwani wapo kwa ajili ya kuwalinda wananchi hao
pamoja na mali zao katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika
Machi 20 mwaka huu.
“Musiwaogope askari, na wala msiwe na wasiwasi, mnapowaona shangilieni
kwani askari ndio msaada wako kwa ajili ya usalama wako endapo inapotokea
vurugu ya aina yoyote, mtaenda kupiga kura salama na mtarudi salama, hakuna
mtu wa kuwabughudhi, msitishwe na mtu yeyote,” alisema Waziri Kitwanga na
kufafanua;
“Leo nazunguka mitaa mbalimbali ya hapa Pemba, lengo ni kuchukua maoni yenu
pamoja na kuwaondolea hofu wananchi na kuwahakikishia vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama vimejipanga vizuri kwa ajili ya kulinda usalama, hivyo
jitokezeni kwa wingi siku ya uchaguzi mkapigie kura kiongozi mnaemtaka.”
Hata hivyo, Waziri Kitwanga alifanya ziara Mkoa wa Kaskazini Pemba katika
msitu wa Ngezi unaodaiwa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi wamejificha katika
msitu huo ili kuokoa maisha yao baada ya kudaiwa kuwa kutatokea na vurugu.
Kitwanga akiongozana na Wakuu wa Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba
pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba, walienda katika msitu huo na
kuukagua na hawakukutana na mtu hata mmoja aliyejificha msituni humo kama
inavyodaiwa na kusambazwa habari na baadhi ya watu wasioitakia mema
Zanzibar.
“Ndugu waandishi wa habari, tumezunguka kwa pamoja kuungalia msitu huu,
kuwatafuta hao wakimbizi, hatujamuona mtu yeyote, ukisikia propaganda ndio hii,
watu hawaitakii mema Zanzibar na Tanzania kiujumla, mmeona kuwa habari hii ni
ya uongo, hakuna mkimbizi yeyote katika msitu huu kama tulivyoshuhudia wote
kwa ujumla,” alisema Kiwanga.
Aliongeza kuwa, baadhi ya wananchi ambao wana mipango yao binafsi wanawatia
hofu wananchi kwa kutunga habari za uongo kuwa Zanzibar imechafuka, wakati
habari hizo hazina uhalisia wowote.
Hata hivyo, wananchi wa Pemba walimuhakikishia Waziri Kitwanga wanafanya
shughuli zao za kuwapatia kipato kama kawaida na pia siku ya uchaguzi wataenda
kupiga kura kama kawaida kwani wanaamini amani itakuwepo kama ilivyokuwa
sasa.
Waziri Kitwanga alifanya ziara Zanzibar katika Kisiwa cha Unguja na
kuzungumza na Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na
Usalama, na baadae kumalizia ziara yake kwa kutembelea katika mikoa yote ya
Pemba ikiwa ni hatua ya kuangalia hali ya usalama visiwani humo katika kipindi
hiki cha uchaguzi mkuu katika maeneo hayo.

No comments:
Post a Comment