Na Beatrice Lyimo-Maelezo
OFISI ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewataka waajiri wote nchini kuhakikisha watumishi wao wanapata Fomu ya wazi ya Mapitio na Upimaji Utendaji Kazi( OPRAS) wa utekelezaji bila usumbufu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kitengo cha mawasiliano cha Ofisi hiyo imeeleza kuwa, kuna baadhi ya Taasisi za Umma watumishi wanaelekezwa kununua fomu za OPRAS kutoka kwa watu binafsi, kitendo ambacho ni kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Fomu za OPRAS haziuzwi hivyo watumishi hawatakiwi kuzinunua, endapo mtumishi atashawishiwa au kulazimishwa kununua fomu hizi atoe taarifa Dawati la Malalamiko Ofisi ya Rais- Utumishi na Utawala Bora ili hatua stahiki zichukuliwe, imefafanua taarifa hiyo.
Pia Fomu hizo zinapatikana katika Tovuti ya Ofisi ya Rais-Menejiment ya Utumishi wa Umma yenye anwani ya www.utumishi.go.tz, hivyo waajiri wanaelezwa kutembelea tovuti hiyo.
Aidha, Serikali ilianzisha matumizi ya mfumo wa wazi wa mapitio na Tathimini ya Utendaji Kazi OPRAS mwezi Julai mwaka 2004 kupitia waraka wa Utumishi Na.2 wa mwaka 2004 na kufuta mfumo wa zamani wa kupima utendaji kazi wa mtumishi kwa njia ya siri.
Mabadiliko ya kutathimini UtendajI kazi wa Watumishi wa Umma kwa uwazi yanakwenda sambamba na Sera ya Menejiment na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 kama ilivyorekebishwa mwaka 2008 na kusisitiza uwekaji wa mifumo ya Menejimenti ya utendaji bora wa kazi inayojali matokeo.
No comments:
Post a Comment