Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio akiongea na waandishi wa habari wakati wa warsha iliyofanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa shughuli za mkondo wa juu (Upstream Operations) kutoka TPDC, Ndugu Kelvin Komba akitoa mada wakati wa warsha ya waandishi wa habari
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Said Meck Sadick akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio na Wakurugenzi wengine kutoka TPDC pamoja na waandishi wa habari.
SEKTA ya gesi na mafuta imeendelea kukua kwa kasi nchini kwetu, ukuaji wa sekta hii unakuja na fursa na changamoto zake. Mojawapo ya changamoto kubwa ni uelewa wa sekta hii kwa wananchi na mategemeo makubwa yaliyopo miongoni mwao. Katika kulitatua hili, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendesha semina ya siku mbili jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kutoa elimu ya mafuta na gesi kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo zaidi wa kuupasha habari umma. Mgeni rasmi katika warsha hiyo alikua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Said Meck Sadick.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dr. James Mataragio alisema “ warsha hii inalenga kuendelea kuwajengea uwezo zaidi waandishi wetu wa habari kuweza kuripoti kwa umahiri na ustadi habari za mafuta na gesi”. Dr. Mataragio aliwashukuru waandishi wa habari kwa juhudi zao za kuupasha habari umma na kuwaasa kwamba kalamu yao ina nguvu hivyo ni vyema ikaendelea kutumika kujenga uchumi wa Taifa kwa kutoa taarifa sahihi kila wakati.
Katika taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji alisisitiza juu ya matarajio yasiyo halisia yaliyopo miongoni mwa wanajamii na kuwaomba waandishi wa habari kusaidia kuwaeleza wananchi juu ya uhalisia wa sekta. Dr. Mataragio alisema kwamba uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi ni wa gharama kubwa na hata mafaniko kwa maana ya mapato makubwa kwa Serikali huchukua muda mrefu kuonekana.
Akitolea mfano mradi mkubwa wa kusindika gesi asilia (Liqufied Natural Gas-LNG), Dr. Mataragio alifafanua kwamba itachukua takribani miaka 8 hadi 10 kabla ya mzigo wa kwanza wa LNG kusafirishwa kwenda katika soko la dunia kwa mauzo. Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC alisisitiza juu ya ushiriki wa wazawa katika sekta hii hususan katika kutoa huduma na kuuza bidhaa. Sheria mpya ya petroli ya mwaka 2015 inawataka wawekezaji wote kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kama ikitokea bidhaa hizo hazipo nchini basi kampuni iingie ubia na kampuni ya kizawa ili kuweza kutoa huduma inayohitajika. Sheria imeeleza kwamba ubia huo lazima umpe mzawa ushiriki usiopunguza asilimia 25%, hii ni fursa kwa wazawa na ni vyema ikachangamkiwa.
Nae mgeni rasmi wa warsha hiyo, Ndugu Said Meck Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisisitiza juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya Taifa kwa kuwa ni mali yetu wananchi wa Tanzania hivyo jukumu la ulinzi ni letu sote. Mkuu wa Mkoa aliyasema haya akilenga ulinzi shirikishi katika miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia ambayo imejengwa na TPDC kwa mkopo kutoka EXIM Bank ya China na kudhaminiwa na Serikali ya Tanzania. Ndugu Said Meck Sadik alisisitiza vile vile juu ya utoaji taarifa mapema pale mtu anapoona kuna hujuma au uharibifu wa aina yoyote katika miundombinu hii, akiongea katika warsha hiyo alisema “miundombinu hii ya gesi na mafuta ni mali ya watanzania hivyo kuilinda ni jukumu letu sote kama wazalendo wa nchii hii”.
TPDC imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ikiwa na lengo la kuongeza uelewa zaidi katika sekta hii mpya na changa ya mafuta na gesi hapa nchini.
No comments:
Post a Comment