HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 14, 2015

WANANCHI WATAKIWA KUWA MAKINI KUELEKEA MSIMU WA CHRISTMAS NA MWAKA MPYA

Na. Tamimu Adam- Jeshi la Polisi

Jeshi la polisi nchini  limewataka wananchi kuimarisha na kutekeleza kwa vitendo dhana ya ulinzi jirani katika kipindi hiki cha kuelekea kuadhimisha sikukuu za  mwisho wa mwaka na kusherekea mwaka mpya kwani  ulinzi jirani ni mkakati madhubuti katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao hapa nchini.

Hayo yalisemwa  na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu mwandamizi wa Polisi Advera Bulimba wakati akitoa tahadhari ya usalama katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka,  ofisini kwake  makao makuu ya Jeshi la Polisi,  jijini Dar es salaam.

“Uzoefu unaonyesha kuwa  kipindi cha kuelekea mwisho  wa mwaka na hususani sikukuu za mwisho wa mwaka  baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo  kujipatia kipato kwa njia isiyo halali kwa kufanya udanganyifu, wizi na utapeli katika maeneo mbalimbali hivyo wananchi wanatakiwa kuwa macho katika shughuli zao” Bulimba alisema. 

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi nchini limejipanga kikamilifu kwa kufanya doria  katika maeneo yote kuhakikisha wananchi wanasheherekea na kumaliza mwaka kwa amani na usalama pasipo hofu yoyote yakufanyiwa vitendo vya uhalifu.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara na wamiliki wa hoteli hapa nchini kuweka kamera na vifaa maalumu vyenye uwezo wa kufuatilia mienendo ya watu wanaoingia na kutoka katika maeneo yao ya biashara ili kuweza kuwabaini wahalifu na uhalifu kwa haraka. 

Pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wanapowatiria shaka watu wasiowafahamu katika maeneo yao kwa  kutoa taarifa kwa namba za bure ambazo ni  111 na 112, namba hizi ni za dhalura na ukipiga katika mkoa wowote ulipo  zitapokelewa na hatua za haraka zitachukuliwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad