Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.
Kutokana na wizi wa umeme kukithiri na kuliingizia hasara Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), Wizara ya Nishati na Madini imeliagiza Shirika hilo
kuimarisha kikosi chake cha ukaguzi wa watumiaji wa umeme ili kubaini wateja
wasio waaminifu wanaoiba umeme na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Badra Masoud
alipofanya mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuendelezea mafaniko na
changamoto katika usimamizi wa sekta ya umeme.
Masoud alisema Wizara inatarajia kuunda kikosi maalum kitakachojumuisha
wataalam kutoka katika taasisi mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo
linalolikosesha mapato shirika la TANESCO.
Alisema kikosi hicho kitajumuisha wataalam kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati
pamoja na vyombo vya usalama na kuongeza kuwa hatua hii imekuja baada ya
Wizara kubaini kuwa kuna baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya
TANESCO kama vile kuchoma nguzo za umeme, kuiba mafuta ya transfoma pamoja
na nyaya za umeme na kuwataka kuacha kufanya hujuma hizo kwani
watakaogundulika wataendelea kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akielezea zoezi hilo, Masoud alisema kuwa hivi sasa sasa vyombo vya dola katika
mkoa wa Lindi vinaendelea kuwasaka na kuwatia nguvuni wale wote waliohusika
kuchoma nguzo za umeme wa msongo mkubwa unaosafirisha umeme kutoka
Mtwara kwenda Lindi katika vijiji vya Hingawali na Njonjo mkoani Lindi na
kusababisha mikoa hiyo miwili kukosa umeme na kusababisha hasara kwa
TANESCO.
Masoud alizitaka Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kuzingatia
matumizi bora ya umeme ili kudhibiti upotevu wa nishati ya umeme na kusisitiza
kuwa utaratibu huu wa matumizi bora ya umeme hufanywa pia na nchi nyingi
duniani kwa ajili ya kukabiliana na upotevu wa umeme.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya taasisi huwa zinaacha umeme ukiendelea kupotea
baada ya muda wa kazi kama vile kuacha viyoyozi, taa, kompyuta na vifaa vingine
vinavyotumia umeme vikiendela kutumia umeme hivyo kusababisha upotevu
mkubwa wa umeme ambao ungetumika katika maeneo mengine au kuokoa fedha
ambazo hutumika kuzalisha umeme huo.
Akielezea hali ya upatikanaji wa umeme nchini Masoud alisema kuwa hali ya
umeme nchini ni nzuri na hakuna mgawo wowote unaoendelea hivi sasa kwani hali
ya uzalishaji ni nzuri pamoja na mabwawa ya maji ambayo hutumika kuzalisha
umeme kukauka.
Alisisitiza kuwa kiasi cha umeme kinachopatikana kwa sasa ni megawati 1500 huku
matumizi ikiwa ni kati ya megawati 800 na 900 kutokana na umeme huo kuzalishwa
kwa kiasi kikubwa kutokana na gesi asilia pamoja na mafuta mazito na dizeli.
No comments:
Post a Comment