HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 21, 2015

WAJENGEENI VIJANA UWEZO WA KUJITEGEMEA-MASAJU

Wanafunzi wakiwa katika pozi na vyeti pamoja na vikombe walivyo zawadiwa.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
WALIMU na viongozi wa shule mbalimbali nchini wamekumbushwa kutoa elimu itakayowajengea uwezo wanafunzi kujitegemea mbali na elimu ya nadharia na vitendo darasani pekee.

Rai hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Bw. George Masaju alipokuwa akiongea wakati wa mahafali ya 8 na maadhimisho ya miaka 10 ya shule ya Patrick Mission High School jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Bw. Masaju ambae alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya kidato cha nne, alisema elimu hiyo ya kujitegemea itawasaidia vijana kujiamini na kupambana katika soko la ajira au kujiajiri wenyewe katika shughuli halali za kuwaingizia mapato.

Alisisitiza pia umuhimu wa kuwafundisha vijana kukua katika mila, tamaduni na maadili bora ya kitanzania kwa ajili ya kudumisha uwepo wa ustawi katika taifa.

“Wafundisheni vizuri historia ya nchi yetu na umuhimu wa kuwa wazalendo wa nchi hii,” alisema Bw. Masaju na kuongezakuwa ‘hakuna taifa lolote duniani lililowahi kuendelea na kuwa na nguvu kubwa kiuchumi na kiutawala ikiwa wananchi wake hawana uzalendo.’

Awali katika taarifa ya shule hiyo ilielezwa kuwa hadi sasa, shule imeshasomesha wanafunzi 100 ambao ni yatima na kila darasa lina yatima wawili.

Bw. Masaju aliipongeza shule hiyo kwa moyo wake wa kusomesha watoto yatima, kwani bila msaada huo, wasingepata elimu.

Miongoni mwa watu aliowashukuru kwa kutoa msaada wa elimu kwa yatima ni Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais Jakaya Kikwete ambaye juhudi zake kupitia Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) pia amekuwa akisaidia shule hiyo.

“Nawaomba watu wengine na taasisi mbalimbali ziendelee kuwasaidia ndugu zetu hawa,” alisema.

Katika sherehe hizo, pia palikuwa na harambee kwa ajili ya kuwasaidia yatima kuweza kupata elimu.

Akitoa ushauri kipindi hiki cha uchaguzi, alisema moja ya mambo yanayoweza kusaidia kutunza amani ya nchi ni kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi.

“Hakuna jambo lolote la umma linalofanywa au kutekelezwa pasipo kuwekewa taratibu za kisheria,” alifafanua.

Alisema ndio maana kutokana na masharti ya sheria mbalimbali, wananchi baada ya kupiga kura wanapaswa kurejea katika makazi yao kusubiria matokeo yatakavyokuwa yanatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia wasimamizi wa uchaguzi au na Tume yenyewe kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais.

Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inakataza katika kifungu chake cha 104 kufanyika kwa mikutano au mikusanyiko siku ya uchaguzi au kufanya mikutano ndani ya umbali wa mita 200 kutoka katika kituo cha kupigia na kuhesabia kura.

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa viongozi wa dini kuwashauri waumini wao kuitii serikali inapokuwa inatekeleza jukumu lake la kusimamia amani, usalama na utengamano katika nchi.

Mmoja wa wazazi katika hafla hiyo, Bw. Ezekiel Marwa aliwataka watoto waliohitimu kutojiingiza katika makundi ya madawa ya kulevya na ulevi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad