HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 21, 2015

SERIKALI KUKOMESHA UCHIMBAJI NA UUZAJI HARAMU WA MADINI

 Kamishna Msaidizi wa Madini, Sehemu ya Leseni, Mhandisi John Nayopa akifungua rasmi warsha kuhusu utekelezaji wa mpango wa kupambana na uchimbaji haramu wa rasilimali kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR)  ujulikanao kama ICGLR Regional Initiative Against Illegal Exploitation of Natural Resources (RINR).

Washiriki wa warsha wakifuatilia uwasilishaji mada kuhusu utekelezaji wa mpango wa kupambana na uchimbaji haramu wa rasilimali kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR)  ujulikanao kama ICGLR Regional Initiative Against Illegal Exploitation of Natural Resources (RINR).
Kamishna Msaidizi wa Madini, Sehemu ya Leseni, Mhandisi John Nayopa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha. Wa kwanza kushoto waliokaa ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Mrimia Mchomvu na wa kwanza kulia ni Muwakilishi kutoka PAC, Stephen Turyahikayo.

 
IMEELEZWA kwamba Serikali imejizatiti katika kuhakikisha inakomesha uchimbaji na uuzaji haramu wa rasilimali ya madini yaliyopo nchini kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
 
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Kamishna Msaidizi wa Madini sehemu ya Leseni, Mhandisi John Nayopa alipomuwakilisha Kamishna wa Madini kwenye ufunguzi wa warsha kuhusu utekelezaji wa mpango wa kupambana na uchimbaji haramu wa rasilimali kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR)  ujulikanao kama ICGLR Regional Initiative Against Illegal Exploitation of Natural Resources (RINR).
 
Mhandisi Nayopa alisema lengo la warsha hiyo ni kufafanua hatua ya utekelezaji  wa mpango wa RINR kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania; kuongeza uelewa wa wadau kuhusu mpango wa RINR,  na kuandaa mpangokazi sahihi ikiwa ni pamoja na mkakati wa utekelezaji wa RINR nchini. 
 
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 12 Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ambazo zimeridhia itifaki zenye lengo la kuimarisha amani, utulivu, demokrasia na utawala bora kwenye nchi husika.
 
Alisema Wakuu wa Nchi 11 za Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) walikutana jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba, 2014 na kukubaliana kwa pamoja kuimarisha maendeleo, usalama na utulivu jambo ambalo anasema linathibitisha dhamira yao ya kubadilisha ukanda wa maziwa makuu kuwa na amani endelevu kwa mataifa hayo na kwa wananchi wake, utulivu wa kisiasa na kijamii na ukuaji wa maendeleo ya pamoja.
 
Mhandisi Nayopa alisema makubaliano hayo yanaitwa Tamko la Dar es Salaam, la Mwaka 2014 ambayo yanajulikana kama The Dar es Salaam Declaration of 2014.
 
“Ili kufanikisha hili, nchi za ICGLR zilisaini  makubaliano (pacts) ambayo yalizaa itifaki mbalimbali na miongoni mwake ni itifaki ya kupambana na uchimbaji haramu wa madini,” alisema Mhandisi Nayopa. 
 
Alisema kwamba mojawapo ya changamoto kuu kwenye baadhi ya nchi za ICGLR ni kukithiri kwa uchimbaji haramu wa madini jambo ambalo linatumika kuchochea migogoro na pia ni chanzo cha fedha kwa wababe wa kivita.
 
Mhandisi Nayopa alisema Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi ambazo zinapasa kuleta maendeleo endelevu kwa jamii na Taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi utakaoleta mabadiliko chanya.
 
“Licha ya mafanikio ambayo Tanzania imekuwa nayo katika kuvutia uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Madini na katika kurasimisha idadi kubwa ya wachimbaji wadogo, lakini bado inakabiliwa na changamoto lukuki,” alisema.
 
Alisema kupitia Mpango huo RINR, Serikali inatarajia matokeo makubwa yenye tija katika kupambana na uchimbaji haramu wa  madini yaliyopo nchini. “Lengo letu na matarajio yetu ni kwamba faida zitokanazo na uchimbaji madini zitaongezeka maradufu na hivyo jamii kwa ujumla kunufaika,” alisema Mhandisi Nayopa.
 
Warsha hiyo ya siku mbili imehudhuriwa na Kamishna Wasaidizi wa Madini kutoka Kanda mbalimbali, watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini hususan kutoka Idara ya Madini, wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, wawakilishi wa wachimbaji wadogo na washirika wa Maendeleo wa Canada wajulikanao kama PartnershiP Africa Canada (PAC). 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad