MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini Tanzania, (TFDA) kwa ushirikiano na Taasisi ya TradeMark East Africa (TMEA) imezindua mfumo wa taarifa za kiutendaji, e-portal ambayo itawezesha TFDA kuhudumia wateja wake kwa mfumo wa kidigitali kwa kutumia mtandao wa internet ambapo sasa huduma za TFDA zitatolewa moja kwa moja kupitia mtandao wa internet hivyo kuleta ufanisi zaidi .
Mfumo unaozinduliwa leo umegharim TFDA takriban Tsh. 300 Milion na kutoka Taasisi ya TMEA imetumia Dola za Marekani $ 250,000 kwa lengo la kuboresha mfumo huo. Uzinduzi huu unahitimisha maboresho yaliyoanza mwaka 2012. Taasisi ya TMEA imeahidi kuendelea kusaidia TFDA kuboresha mifumo yake ya usimamizi wa huduma za kimaabara. Msaada wa ziada utaelekezwa kwenye kuinganisha TFDA na Tasisi za kifedha ili kuboresha mifumo ya malipo kwa njia ya mtandao. Na hatua ya mwisho ni TMEA itasaidia kuuingiza TFDA kwenye mfumo wa malipo yote nchini Tanzania, kupitia dirisha moja la kitaifa (National Single Window), mradi ambao uko kwenye maandalizi.
Akizungumza katika uzinduzi Dkt. Donan Mmbando, Katibu Mkuu Wizara ya Afya alisema,
“Mfumo huu unaozinduliwa leo utarahisisha katika kufanya maamuzi ya kiudhibiti kwa maeneo ya utoaji wa vibali ya kuingiza bidhaa nchini na kutoa bidhaa nje ya nchi kwa kuwa muda wa kuandaa vibali utafupishwa.
Hata hivyo mfumo huu utasaidia katika kuhudumia wateja kwa ufasaha katika kusajili na ufuatialiaji wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba nchini. Ubunifu huu utasaidia kuongeza idadi ya wateja kufuata na kukidhi matakwa ya kisheria katika udhibiti hivyo kuimarisha usalama na ubora wa bidhaa zilizopo katika soko”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti B. Sillo aliongeza,
"TFDA inaishukuru sana TMEA kwa msaada wake kwa TFDA katika uanzishwaji wa e- portal, ambayo itarahisisha ukusanyaji wa takwimu, uchambuzi na uhifadhi wa taarifa za usajili, uratibu na ufuatiliaji wa taarifa za vyakula, madawa, vipodozi, vifaa tiba na kuyafuatilia maduka ya dawa nchini Tanzania. Hii itaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na itarahisisha muda wa kazi na kurahisisha kufikia maamuzi.”
Mkurugenzi wa TradeMark East Africa Tawi la Tanzania Dk Josephat Kweka aliongeza,
"Portal hii inatarajiwa kuongeza kasi ya usajili, kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi na muda wa kupeleka bidhaa nje ya nchi, hivyo kuboresha mazingira ya kufanya biashara!. TMEA Tumefurahi kushirikiana na TFDA shirika ambalo kiungo katika kulinda na kuboresha bidhaa za afya ya umma wa Watanzania, huku ikihakikisha ufanisi wa viwango vya ubora na usalama wa bidhaa za vyakula, madawa, vipodozi na vifaa tiba. "
Umuhimu wa hii e-portal ya TFDA, itawezesha wafanyabiashara kuomba na kupata vibali vyote muhimu, kwa njia ya mtandao, bila kulazimika kufika TFDA, na wakati huo huo, pia utawawezesha maafisa wa TFDA, kupitia maombi hayo, kuyakagua na kuyaidhinisha kidigitali, kwa njia ya mtandao, ambapo huduma sasa zitatolewa usiku na mchana, sasa 24 kwa siku zikiwemo Jumamosi, Jumapili na sikukuu. (24/7) .
Huduma hizi zitaunganishwa na mtandao wa Mfumo wa Taifa wa Malipo kupitia Dirisha Moja (National Electronic Single Window) ambao uko kwenye maandalizi.
Mfumo huu mpya wa kidigitali unaojiendesha wenyewe, utaboresha kasi ya utoaji wa vibali vya TFDA kuagiza, kuingiza na kusafirisha nje ya nchi, bidhaa za vyakula, madawa, vipodozi na vifaa tiba, hivyo kuimarisha uwezeshaji wa biashara.
Portal hii imewezeshwa na TMEA kama sehemu ya majukumu yake ya kukuza biashara ya kikanda na ushirikiano wa kiuchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
e-Portal hii ya TFDA ni mtandao unaotumia Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (ICT) na inajumuisha ya Mfumo wa Management Information System (MIS) kwa watoa huduma, na Trade Portal kwa wapokea huduma ambao ni wafanya biashara. Uwezeshaji huu kwa TFDA, kwa msaada wa TradeMark East Africa (TMEA), unalenga kuwezesha TFDA kuwahudumia wateja wake kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.
TFDA imeanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Kiutendaji kutumika kwa ajili ya ukusanyaji wa takwimu, uhifadhi na uchambuzi wa taarifa kuhusu usajili, kanuni na ufuatiliaji wa vyakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na maduka ya dawa nchini Tanzania. Mfumo huu, utaongeza ufanisi katika utoaji wa maamuz na urahisishaji kazi ya usimamizi. Aidha, e- portal itashughulikia maombi ya leseni za kuagiza na kuuza bidhaa kwa njia ya mtandao, (online).
Matokeo yanayotarajiwa kutokana na e- portal hii ya TFDA ni online ni pamoja na:
• Kuongezeka kwa ufanisi kwa njia ya kuokoa muda wa kufanya biashana na kupunguza gharama kwa kwa wadau, kufuatia kuthitajika uwepo wa mtu wala hati katika ofisi za TFDA.
• upatikanaji wa taarifa na nyaraka kwa urahisi kwa kuingia mara moja tuu kwenye mtandao.
• Kuongezeka kwa viwango vya ufuatiliaji.
• Kuongezeka kwa ubora wa huduma, uwazi na uwajibikaji katika huduma zinazotolewa na TFDA
No comments:
Post a Comment