KUSOMA ZAIDI links goes to sheriayakub.blogspot.com
Na Bashir Yakub.
Kawaida wanandoa wengi wanapoingia katika migogoro moja ya jambo wanalokimbilia kama jawabu la mgogoro ni talaka.
Kwa misingi ya ndoa za kiislamu talaka huruhusiwa tofauti na misingi ya ndoa za kikiristo ambazo talaka huwa haziruhusiwi.
Hata hivyo hata kama ndoa ni ya kikristo ambayo hairuhusu talaka linapokuja suala la mahakama basi hata ndoa hizo nazo hutolewa talaka. Ieleweke kuwa kwa mujibu wa Sheria Ya Ndoa ya 1971 suluhu ya kumaliza utata katika ndoa si talaka tu.
Na hii ni kutokana na umuhimu wa ndoa. Katika hili sheria ya ndoa imetoa chagua jingine ambalo mtu anaweza kulitumia kama mbadala wa talaka. Hili linahusu kutengana kama tutakavyoona.
1.KUTENGANA KISHERIA.
Kutengana kwa mujibu wa sheria ni hatua ambapo watu wawili mwanamke na mwanaume walio katika ndoa halali huamua kutoshirikiana katika mambo kadhaa ya kindoa huku ndoa ikihesabika kuwa haijavunjika. Katika hili kinachositishwa ni baadhi ya haki na wajibu wa kindoa. Lakini kusitishwa kwa wajibu na haki hizo hakuhesabiki kuwa kumevunja ndoa.
2. AINA ZA KUTENGANA KISHERIA.
Kisheria zipo njia mbili ambazo wanandoa wanaweza kutumia ili kutengana. Kwanza ni kuwa wanandoa wanaweza kutengana wenyewe kwa hiari yao . Kutengana kwa hiari ni kuwa wanakubaliana kutengana kwa muda fulani kutokana na kutoelewana kwasababu mbalimbali za kifamilia.
Pili wanaweza kutengana kwa kutenganishwa na mahakama kwa mujibu wa kifungu cha 99 cha sheria ya ndoa 1971. Hii ni baada ya mmoja wa wanandoa kuiomba mahakama iwatenganishe kwa kipindi fulani na mahakama kuridhika kuwa ipo haja hiyo. Mara nyingi kutengana kwa njia ya mahakama hutokea baada ya hatua za kutengana kwa hiari kushindikana. Mara kadhaa hutokea ambapo mmoja wa ndoa huwa amekerwa na baadhi ya tabia na hivyo kumuomba mwenzake watengane ambapo mwenzake hukataa. Inapotokea hivyo ndipo mwanandoa anapolazimika kukimbilia mahakamani kuomba kutengana.
3. TOFAUTI YA KUTENGANA NA TALAKA.
Talaka ni hatua ambapo ndoa hutangazwa kuwa imevunjika kabisa na kila mmoja hutakiwa kuendelea na maisha yake. Talaka huambatana na haki ikiwemo ile ya mgawanyo wa mali. Wakati kutengana ni hatua ya kuchana kwa muda na kurudiana baadae. Kutengana hakuambatani na haki ya kugawana mali za machumo ya wanandoa.
4. UMUHIMU WA KUTENGANA BILA TALAKA.
Sheria imeelekeza tendo hili la kutengana kwa kuzingatia maslahi mapana ya wanandoa, familia na jamii kwa ujumla. Lengo kuu la hatua ya kutengana ni kutoa nafasi kwa walengwa wanandoa kujirekebisha . Inaaminika kuwa katika kipindi ambacho wanandoa hutengana huwa kuna mwanya mkubwa ambao hupelekea kurekebisha baadhi ya tabia ambazo zilikuwa kikwazo. Kutengana ni nafasi ya mtu kujirudi.
5. MATUNZO YA MWANAMKE NA WATOTO KIPINDI CHA KUTENGANA.
Kwa upande wa mwanaume ni lazima kwake kuendelea kutoa matunzo ya mwanamke pamoja na ya watoto kama wapo. Kisheria mwanaume ndiye huwajibika kutoa matumizi ya watoto pamoja na kumtunza mke wake. Katika kipindi cha kutengana haki na wajibu huu huendelea mpaka kipindi cha kutengana kitakapoisha. Hata hivyo yapo mazingira ambapo mwanamke anaweza kutakiwa kutoa matunzo kwa mwanaume kama itakavyokubaliwa katika masharti ya kutengana.
6. MUDA WA KUTENGANA.
Kawaida (practice) muda wa kutengana unaotakiwa inabidi iwe miaka miwili na ikizidi isizidi mitatu. Ikiwa muda huo utapita bila muafaka kwa wahusika basi hatua za talaka zinaweza kufuata.
7. KUAMUA KUSITISHA MUDA WA KUTENGANA.
Kifungu cha 113 ( 1 ) kinatoa uhuru kwa wanandoa kutuma maombi ya pamoja mahakamani kuomba kusitishwa kwa amri ya kutengana. Hii ni ikiwa kutengana kulitokana na amri ya mahakama. Ikiwa kutengana hukukutokana na mahakama ila ilikuwa kwa ridhaa ya wanandoa basi wahusika kwa hiari yao wanaweza kuamua kusitisha bila kuhitaji amri ya mahakama.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment