Waziri Mkuu wa Mstaafu na Mbunge wa Monduli,Mh. Edward Lowassa amewanyooshea vidole viongozi wa kimila wa kabila la wamasai (malaigwanani),viongozi wa vijiji na wale wa CCM wilayani humo, kuwa wanalaumiwa kwa kushiriki katika uuzaji ardhi kinyume na sheria.
Akifungua semina ya siku mbili ya juu ya maswala ya ardhi kwenye ukumbi wa hoteli ya Emanyata mjini Monduli,Mh. Lowassa amesema shutuma hizo zimekuwa nyingi kwa viongozi hao kwa kuuza utajiri (ardhi) na kununua umasikini.
"Walikuja pale nyumbani kwangu wale watu wa maombezi (walokole), moja ya mambo waliyoyalalamikia ni uuzwaji holela wa ardhi,wakaniambia hivi Mh. Mbunge hamuoni viongozi wa vijiji na wa CCM pamoja na malaigwanan wanavyopokea rushwa na kuuza ardhi?Wanavyowadhulumu wajane?" Alisema Lowassa na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa kulijadili kwa kina suala hilo.
Kutokana na hali hiyo Lowassa amewatahadharisha viongozi wa vijiji kuhakikisha wanaiondoa kero hiyo, kabla ya uchaguzi ujayo wa serikali za mitaa vinginevyo tatizo hilo litawagharimu.
Aidha Lowassa ambaye ameshirikiana na mbunge wa Viti maalum (CCM),Namelok Sokoine ndiyo walioiandaa semina hiyo, amempongeza mbunge wa zamani wa Monduli hayati Edward Moringe Sokoine, kwa kufanikisha makubaliano kati ya wilaya na jeshi kuhusiana na matumizi ya ardhi.
"Marehemu Sokoine alifanya jambo kubwa sana kwa kufikia makubaliano yale na faida yake kwetu sisi wana Monduli ni kubwa,kimejengwa hapa Chuo kikubwa cha kijeshi (TMA), na tulikubaliana tusilipwe fidia na jeshi ili tuwe na haki kwa mifugo yetu kuingia eneo lile,lakini kuna watu wameipeleka halmashauri mahakamani kupinga" alisema na kuonya kuwa" tutapambana kuhakikisha tunashinda! tumekuwa na mahusiano mazuri na jeshi na tunataka mahusiano hayo yaendelee".
Naye mbunge wa viti maalum,Nameloki Sokoine alisema kuwa madhumuni ya kuandaa semina hiyo ni kutoa dira itakayofafanua nini kifanyike kuondoa tatizo hilo la uuzaji holela wa ardhi.
Amesema mifugo na binadamu wamekuwa wakiongezeka lakini ardhi ni ile ile kwa hivyo bila ya kuwepo kwa dira na mipango thabiti hali itakuwa mbaya.
Aidha alitoa changamoto kwa mbunge wa Monduli Mh. Lowassa kusaidia kupatikana kwa wawekezaji wa viwanda vya maziwa, ngozi na nyama wilayani Monduli.
"Ningependa kumuomba Mh. Mbunge najua hili analiweza atusaidie watu wa Monduli tupate wawekezaji wa viwanda vya ngozi, maziwa na nyama,tukiwa na viwanda hivi itasaidia wafugaji kuachana na ufugaji wa kimila wa ng'ombe wengi an badala yake kuwa na ng'ombe wachache wa kisasa wenye tija" alisema Namelok na kushangiliwa.
Waziri mkuu wa Mstaafu na Mbunge wa Monduli,Mh. Edward Lowassa akihutubia wakati wa semina ya kwa wakazi wa Monduli juu ya maswala ya ardhi katika hoteli ya Emanyata,Wlayani humo.ambapo alisema kuuza ardhi ni sawa na kuuza utajiri na kununua umasikini.Wilaya ya Monduli ni moja kati ya wilaya zenye matatizo makubwa ya ardhi.
Mbunge wa Monduli viti maalum,Namelok Sokoine akikabidhi sehemu ya baiskeli 100 alizotoa kwa watendaji wa Kata na kijiji wilayani humo,ili kuimarisha uhai wa Chama.Alikabidhi msaada huo wakati wa semina maalum juu ya ardhi wilayani Monduli.
No comments:
Post a Comment