HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 10, 2014

Mh. Muhongo ataka madhehebu ya dini kutumia fursa za nishati, madini

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akieleza jambo wakati wa kikao baina yake na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini za Kiislamu na Kikiristo kutoka Mikoa ya Mwanza na Geita. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja na baadhi ya Maafisa wa Wizara.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akisalimiana na Askofu Zenabius Isaya na baadhi ya Viongozi wa Dini wa Kamati ya Amani kutoka Mikoa ya Mwanza na Geita. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja na baadhi ya Maafisa wa Wizara.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, akisalimiana na Sheikh Hassan Kabeke mara baada ya kikao kilichojadili masuala mbalimbali kuhusu Wizara baina yao. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja na baadhi ya Maafisa wa Wizara.

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo katika picha ya pamoja na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini za Kiislamu na Kikirsto kutoka Mikoa ya Mwanza na Geita. Wa pili nyuma kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Sheria Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani.

Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amewataka Viongozi wa Dini kuona umuhimu wa kuwa na vyanzo vya kiuchumi kupitia sekta za Nishati na Madini kutokana na kuwepo kwa fursa za kutosha kwenye  sekta ya umeme.


Waziri Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini za Kiislamu na Kikristo kutoka Mikoa ya Mwanza na Geita waliofika Wizarani kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Wizara.


“Madhehebu ya dini jipangeni muwe na vyanzo vyenu vya kiuchumi. Mbali na kusaidia kuleta amani katika jamii zetu, tumieni fursa zilizopo kiuchumi kupitia nishati na madini. Fursa zipo, lifanyieni kazi jambo hili,” alisisitiza Profesa Muhongo.


Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Ngosi Mwihava na Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja, Profesa Muhongo alisema kuwa, mkakati wa Wizara ni kuhakikisha kwamba inafikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 kwa kuhakikisha kwamba, Tanzania inavuka katika hali ya sasa kiuchumi na kuingia katika uchumi wa kati kwa kupitia sekta ya nishati na madini.


Aidha, alisema kuwa, umaskini wa Tanzania unaweza kufutwa kwa kupitia sekta ya nishati na madini kutokana na umuhimu wa sekta hizo kwa maendeleo ya nchi,  kwani  kuna mchango mkubwa wa sekta hizo katika kutengeneza ajira na kuwezesha mazingira bora kiuchumi.


“Tuko hapa kuwatumikia wananchi. Wizara na Taasisi zilizo chini yetu zitawatumikia wananchi.  Tumekataa rushwa na hatutachukua rushwa. Wizara hii ndio roho ya nchi hii.  Malengo yetu ni kufikia maendelo ya kiuchumi bila rushwa, alisema Waziri Muhongo.


Akizungumzia suala la nishati ya umeme, alieleza kuwa, mkakati wa Wizara ni kuhakikisha kwamba Tanzania inakua na umeme wa kutosha na nafuu kwa watanzania wote. “Tunataka kuwa na umeme wa kutosha,tunataka kuzalisha umeme mwingi nafuu,”alisisitiza Muhongo.


Akizungumzia madini Profesa Muhongo aliwataka viongozi wa dini kuwahamasisha wachimbaji wadogo kujiunga katika vikundi vidogo vidogo na katika vyama vya wachimbaji ili wizara iweze kuwafikia kwa kuwapitia ruzuku na kuongeza kuwa, lengo ni kuwafanya wachimbaji hao kuwa wachimbaji wa kati.


Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Paul Masanja alitoa rai  kwa viongozi hao kuwaelimisha wananchi wanaowazunguka kuhusu umuhimu wa wachimbaji wadogo  kujiunga katika vikundi vidogo na kuongeza kuwa, wanayo nafasi kubwa itakayosaidia mazingira rafiki ya kufanya kazi katika sekta hiyo.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya dini za Kikirsto na Kiislamu, Sheikh Hassan Kabeke alieleza kuwa, Kongamano la viongozi wa dini lililofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Januari, 2014 lilisaidia kufungua uelewa wa viongozi hao kuhusu sekta ya nishati na madini na hivyo kuona umuhimu wa viongozi wengine Kanda ya Ziwa kuelimishwa kuhusu sekta hizo kutokana na ukanda huo kuwa na uwepo wa rasilimali nyingi za madini.


“Kanda ya ziwa tunahitaji kuzifahamu fursa za wizara hii, tunahitaji elimu, tunataka Wizara mkutane na viongozi wenzetu muwaelimishe” aliongeza Sheikh Kabeke.


Katibu wa Kamati ya Amani ya dini za Kikirsto na Kiislamu, Askofu Zenabius Isaya alieleza kuwa wamefunguliwa macho na Kongamano la Dar es Salaam lililofanyika Januari, 2014 tofauti na walivyokuwa wakisikia awali. “Mnafanya vizuri sana. Mambo ya Mtwara yanasikika maendeleo yake tunayasikia,”aliongeza.


Aidha, viongozi hao walichukua fursa hiyo kuipongeza Wizara kutokana na utendaji wake na dhamira yake ya kuhakikisha Tanzania inazalisha kiasi cha kutosha cha umeme ikiwemo mkakati wake wa kuinua nchi kiuchumi kupitia sekta za nishati na madini.


Aidha, katika kikao hicho iliafikiwa kufanyika kwa Kongamano la Viongozi wa Dini Kanda ya Ziwa tarehe 26-27 Novemba, 2014, ambapo viongozi hao wataelimishwa masuala mbalimbali kuhusu Wizara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad