Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Wataalamu kutoka nchi za Zambia, Kenya na Tanzania kutoka Wizara zinazoshughulika na masuala ya nishati wameanza majadiliano ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi za nchi hizo. Kikao cha Majadiliano hayo kiliongozwa na Makatibu Wakuu kutoka katika nchi husika na kitafuatiwa na mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 30 Septemba, 2014 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi amezitaka nchi hizo kuunga mkono jitihada za utekelezaji wa mradi huo kutokana na umuhimu wake kiuchumi ikiwemo kuhakikisha nchi hizo zinakuwa na nishati ya umeme ya kutosha.
Aidha, ameongeza kuwa, tayari Tanzania imeanza kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inaanza utekelezaji wa mradi huo ambao umechukua kipindi kirefu kuanza kutekelezwa na kuongeza kuwa, Tanzania iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kuhakikisha kwamba mradi huo unafanikiwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Petroli Kenya Mhandisi Richard Mwiru, ameeleza kuwa, kuna matokeo bora yatakayotokana na utekelezaji wa mradi huo, matokeo ambayo yatasaidia biashara ya umeme na upatikanaji wa umeme rahisi kwa nchi hizo. Aidha, ameongeza kuwa, nchi ya Kenya iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Migodi,Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia, Charity Mwansa, ameeleza kuwa, anatarajia mkutano huo utatoa fursa zitakazosaidia utekelezaji wa mradi huo kuendelea kutoka mahali ulipofikia ili kuweza kutoa matokeo chanya yatakayokuwa na manufaa kwa nchi hizo ukizingatiwa kuwa, nchi hizo zimebahatika kuwa na rasilimali asilia za kutosha.
Aidha, Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika anayeshughulikia miradi (COMESA), Dkt. Kipyego Cheluges amezitaka nchi hizo kuhakikisha kwamba mradi huo unatekelezwa kutokana na manufaa ambayo nchi hizo zitayapata ikiwemo bara la Afrika na kuongeza kuwa, COMESA itashirikiana kwa karibu na nchi hizo kuhakikisha kwamba, mradi unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, akiongea wakati wa kikao cha Wataalamu kutoka nchi za Zambia, Kenya na Tanzania Kujadili Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi za nchi hizo. Wengine kutoka kushoto ni Balozi wa Zambia nchini Judith Kapijimpanga, Katibu Mkuu Wizara ya Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji Zambia, Charity Mwansa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Petroli Kenya, Mhandisi Richard Mwiru na Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Soko la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika anayeshughulikia miradi (COMESA), Dkt. Kipyego Cheluges.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Petroli Kenya, Mhandisi Richard Mwiru (wa pili kulia) akiongea jambo wakati wa kikao hicho, ambapo ameeleza utayari wa nchi ya Kenya katika utekelezaji wa mradi huo.
Sehemu ya Wataalamu kutoka nchi za Zambia, Kenya na Tanzania wakifuatilia kikao cha Kujadili Utekelezaji wa Mradi wa Kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi za nchi hizo.
Mtaalamu Mwelekezi kutoka nchi ya Zambia Siyanga Zomba, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji na hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kuunganisha Mtandao wa Umeme katika Gridi kwa nchi za Zambia, Kenya na Tanzania.
No comments:
Post a Comment