Na Frank Geofray – Jeshi la Polisi, Moshi.
Askari Polisi kote nchini wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii, kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha na kuboresha uhusiano mwema na jamii ambao utasaidia kukabiliana na vitendo vya uhalifu na wahalifu vinavyojitokeza hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Nchini, Abdulrahman Kaniki wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Maafisa wanadhimu, wahasibu na watunza stoo kutoka mikoa na vikosi vya Jeshi la Polisi kote nchi ni unaoendelea mkoani Kilimanjaro katika chuo cha Polisi Moshi (CCP) ukiwa na kauli mbiu isemayo usimamizi wa raslimali ni tunu ya Jeshi la Polisi kwa maendeleo yake.
Kaniki alisema askari wote wanapaswa kutoa huduma bora kwakuwa wananchi ndio wanaotoa tathmini ya huduma zinazotolewa na jeshi hilo hivyo wananchi watakapopata huduma bora wataendelea kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwabaini wahalifu wanaoishi nao katika jamii inayowazunguka.
Pia amewataka washiriki wa mkutano kutumia fursa waliyoipata katika kuweka mipango ya pamoja itakayosaidia kupunguza uhalifu na kuhimarisha amani na utulivu unaoendelea hapa nchini ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa bajeti ya jeshi la Polisi.
Aidha amewapongeza askari kwa utendaji wao wa kazi ambao umesaidia nchi kuwa katika hali ya amani na utulivu licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Kwa upande wake Kamishna wa fedha na logistiki Clodwig Mtweve, alisema lengo la mkutano huo ni kutathmini hali ya utendaji wa Jeshi la polisi na kutafutia ufumbuzi changamoto zinazolikabili hasa katika upande wa rasilimali.
“Kupitia mkutano huu utaboresha mipango yetu katika matumizi ya raslimali tulizonazo na kuhakikisha zinaleta tija kama ilivyokusudiwa jambo ambalo ni muhimu katika maendeleo ya Jeshi letu la Polisi.”Alisema Mtweve.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki (kushoto) akielekea kufungua mkutano wa Maafisa wanadhimu, Wahasibu na watunza stoo wa Jeshi la Polisi kutoka Mikoa na Vikosi vya Polisi kote Nchini unaofanyika katika Chuo cha Polisi Moshi.Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi Dkt.Ibrahim Msengi na Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi, Matanga Mbushi.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa Maafisa wanadhimu, Wahasibu na watunza stoo wa Jeshi la Polisi wakiwa wanafuatilia hotuba ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika katika Chuo cha Polisi Moshi.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki (katikati) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Dkt.Ibrahim Msengi wakati wa ufunguziwa mkutano wa Maafisa wanadhimu, Wahasibu na watunza stoo wa Jeshi la Polisi kutoka Mikoa na Vikosi vya Polisi kote Nchini unaofanyika katika Chuo cha Polisi Moshi. Kushoto ni Kamishna wa fedha na logistiki Clodwig Mtweve.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
No comments:
Post a Comment