Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akiangalia maporomoko ya maji yaliyopo kwenye hifadhi ya taifa ya Kitulo.
=====
Na Edwin Moshi, Makete.
Hifadhi
ya taifa ya Kitulo iliyopo wilayani Makete mkoani Njombe imejipanga
vilivyo kuongeza vivutio vipya vya utalii hifadhini humo pamoja na
kuboresha miundombinu ya barabara na njia za kupita watalii ili
wafurahie vivutio vilivyopo hifadhini humo.
Akizungumza
mbele ya kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Makete iliyofanya ziara
hifadhini humo, Kaimu mkuu wa hifadhi ya Kitulo Bw.Pius Mzimbe (pichani
juu) amesema kwa hivi sasa wanazidi kuboresha zaidi hifadhi hiyo ambapo
kwa mwaka huu wa fedha 2014/2015 wataboresha barabara zilizopo kwenye
hifadhi hiyo ili kusaidia kufikika kirahisi kwa vivutio lukuki
vinavyopatikana kwenye hifadhi hiyo hasa kwenye maporomoko ya maji
pamoja na kujionea mimea ya aina mbalimbali iliyoota kwenye hifadhi
hiyo.
"Kwa
mfano kwa sasa tunajenga camp site (vituo vya kupumzikia watalii)
ambapo watalii wakiwa hapa watajionea mandhari mabalimbali ikiwemo
milima, mimea na vingine, watapanda kwenye milima na kuona maeneo ya
mbali na wakichoka watarudi hapa kupumzika na tutawawekea bafu na
maliwato kwa ajili yao pamoja na jiko kwa ajili ya kuwapikia vyakula
wanavyovipenda hasa vya asili" alisema Mzimbe.
Amesema
kumekuwa na changamoto ya kutofikia baadhi ya vivutio hasa maporomoko
ya maji kutokana na ubovu wa barabara wakati wa masika hivyo kwa
kuziboresha kutasaidia barabara hizo kupitika muda wote hivyo kuongeza
mapato yatokanayo na hifadhi hiyo ya Kitulo.
Bw.
Mzimbe ametoa wito kwa wananchi wa ndani na nje ya Makete kujijengea
utaratibu wa kutembelea hifadhi hiyo ili wajionee vivutio mbalimbali
ikiwemo maua, ndege, maporomoko ya maji na mimea mbalimbali ambayo ipo
hifadhini humo tu na vivutio vingine ambavyo wanavigundua siku hadi
siku.
Kwa
upande wake mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati
ya ulinzi na usalama wilaya Mh. Josephine Matiro amesema wilaya yake
imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii ambavyo vipo ndani ya
hifadhi ya Kitulo na vingine vipo nje hivyo wao kama serikali
watahakikisha vivutio hivyo vinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na cha baadaye.
Mh.
Matiro amesema ni vyema wanamakete wakajitokeza kwa wingi kufanya
utalii wa ndani na kujionea jinsi wilaya yao ilivyobarikiwa na ni jambo
la aibu kwa watalii wa nje ya nchi kuja kutembelea hifadhi ya Kitulo
ilihali wakazi wa makete hawajawahi kuitembelea.
"Kwa
mfano leo tumejionea vivutio vingi humu hifadhini, lakini ukipita kwa
gari unaishia kuona maua ama ndege lakini ukiingia humu ndani vipo
vivutio vingi vya ajabu na vya kuvutia, mimi na kamati ya ulinzi na
usalama tumeamua kuonesha mfano, tunaomba wananchi mtuunge mkono kwa
kuja kuitembelea hifadhi yetu ya kitulo" alisema Matiro.
Wakiwa
hifadhini humo wajumbe wametembelea maporomoko ya maji ya Mwakipembo na
Numbwe ambayo ni marefu zaidi, pamoja na eneo ambalo linajengwa vituo
vya kupumzikia watalii na pia kujione mandhari tulivu ya hifadhi hiyo ya
Kitulo.
Hifadhi
ya Kitulo ipo katika tarafa ya matamba wilayani Makete na inasifika
duniani kwa kuwa na maua na ndege na kwa hivi sasa vivutio vingine vya
utalii vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.
No comments:
Post a Comment