HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 27, 2013

Wafanyakazi NHIF jitumeni bila kujali muda - Balozi Mchumo

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Balozi Ali Mchumo akifungua baraza la Wafanyakazi wa Mfuko huo mjini Bagamoyo.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba (kushoto) na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Beatus Chijumba wakifuatilia nasaha za Mwenyekiti.
Naibu Mkurugenzi Mkuu, Hamis Mdee akitoa neon la shukrani kwa hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi.
Wawakilishi wa watumishi wa Mfuko wakifuatilia hotuba.
Watumishi wakifuatilia nasaha za ufunguzi.
Balozi Mchumo na Mkurugenzi Mkuu wakifuatilia dondoo za mada zitakazojadiliwa na Baraza hilo.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia jambo.
Picha ya pamoja ya Mwenyekiti wa Bodi na Menejimenti ya Mfuko.

Na Grace Michael

WATUMISHI wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wametakiwa kufanya kazi bila kujali muda wao wa kazi waliopangiwa kutokana na umuhimu wa majukumu waliyokabidhiwa ya kutoa huduma za matibabu kwa wanachama na kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa kwenye utaratibu wa bima ya Afya.

Akifungua Baraza Kuu la Wafanyakazi mjini Bagamoyo leo, Mwenyekiti wa Bodi wa NHIF, Balozi Ali Mchumo, alisema kuwa ili lengo la kuwafikia watanzania wengi na wanachama wa Mfuko huo kupata huduma zilizo bora ni vyema wafanyakazi wakaendeleza utamaduni walioujenga wa kufanya kazi kwa kujituma bila kujali kumalizika kwa muda wa kazi uliopangwa.

“Historia mliyoijenga ya kufanya kazi bila kuchoka ni vyema mkaiendeleza, jukumu tulilokabidhiwa ni kubwa na zito hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anajituma na kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kazi,” alisisitiza Balozi Mchumo.

Akizungumzia uimarishaji wa shirika hilo, aliagiza watumishi hao kuhakikisha wanajiridhisha katika mambo yote hususan ya uhakiki wa madai ya watoa huduma kutokana na kuwepo kwa udanganyifu wa madai unaofanywa na baadhi ya watoa huduma ili kuhakikisha fedha zinazolipwa na Mfuko zinalipwa kwa matumizi halali ya wanachama na si vinginevyo.

Kuhusu suala la nafasi za wategemezi kwa mwanachama mchangiaji, alisema kuwa mwongozo uliotolewa unaoelekeza wategemezi wa mwanachama ufuatwe ili huduma inayotolewa na Mfuko inawahusu walengwa moja kwa moja ambao ni Mke au mme, watoto na wazazi wa mwanachama mchangiaji.

“Hakikisheni huduma inakuwa ni kwa walengwa na hata uandaaji wa vitambulisho ufanyike kwa makini na kujiridhisha zaidi ili kitambulisho kitolewe kwa mlengwa ambaye ametimiza matakwa ya kuwa mtegemezi au mnufaika wa Mfuko,” alisema.

Balozi Mchumo alikwenda mbali zaidi kwa kuwataka watumishi wa Mfuko huo kuhakikisha wanaendeleza dhana ya ushirikishanaji ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi.

Kwa upande wa Bodi, alisema itahakikisha inalipa kipaumbele suala la kuuelimisha umma kuhusiana na dhana ya bima ya afya ili kutimiza malengo yalipo ya Watanzania kujiunga na NHIF/CHF.

Naye Naibu Mkurugenzi wa NHIF, Hamis Mdee wakati akitoa neno la shukrani alisisitiza zaidi kuzingatia maagizo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi kutokana na ukweli kwamba Watanzania wanayo matumaini makubwa na Mfuko hasa katika utoaji wa huduma za matibabu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi, Baraka Maduhu, alisema kuwa ni vyema wafanyakazi wakatambua kuwa haki na wajibu ni vitu vinavyokwenda sambamba hivyo kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake ipasavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad