HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 6, 2013

TAMKO LA RAIS KIKWETE JUU YA TUKIO LA MLIPUKO WA BOMU JIJINI ARUSHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa. Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake.

Rais Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.

Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu. Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.

Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.

Rais Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013

4 comments:

  1. Tunaamini Mh Rais ana nia ya dhati na alichokisema.Tamko pekee halitoshi manake nchi matamko yanatolewa mengi sana lakini matokeo yake kivitendo hayaonekani. Jambo hili ni zito na linahusisha Diplomatic Figure hivyo serikali ijitahidi kuchukua hatua madhubuti

    ReplyDelete
  2. Sina hakika na maneno yaliyotolewa na mheshimiwa Rais wa Tanzania kama yanabeba nia ya kweli ya kushughulikia tatizo hili. Hofu yangu ni kwamba ikiwa serikali itaendelea kulegalega katika kushughulikia matukio kama haya basi kuna wakati ambapo vitajitokeza vikundi vingine kwa ajili ya kulipiza kisasi. Serikali ionyeshe msimamo ili kila raia na mgeni atambue msimamo wa serikali juu ya hilo

    ReplyDelete
  3. Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuonesha huruma na moyo wa kuwajali Watanzania. Ninaamini atafanya zaidi ya hapo kwa kuahirisha zaira yake nchini Kuwait na kurudi haraka nchini kuongeza nguvu katika kuwasaka wahatarisha amani na usalama wa Tanzania.

    Tunaamini kuwa, sasa anayoyakuzungumza na kuwawajibisha watendaji wa serikali yake juu ya matukio yanayoendelea sasa katika nchi na kukosekana juhudi na utashi wa kisiasa ktk kushughulikia uhalifu na matatizo mengine ya Watanzania.

    Tunatamani kuona kwa vitendo moyo wa kujali toka kwa kiongozi wetu wa nchi. Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani na IGP waoneshe pia utashi wao wa kisiasa na kiutendaji, kwani ndani ya muda mfupi yametokea mambo mengi ya kuhatarisha amani na usalama wa Watanzania na wao wakiwa madarakani. Wakati umefika kwa wao kuonesha uzalendo wa kweli na kukiri juu ya uwezo wao katika kushughulikia uhalifu hapa nchini.

    Wahatarisha amani ya nchi yetu inaelekea wamejifunza kwa muda mrefu juu ya uwezo wa watendaji na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na wakaona upo uwezekano wa wao kufanya shughuli zao kwa uhuru mkubwa bila bughudha yoyote, na hivyo wakafikia kutekeleza azma yao.

    Wapendwa Waziri Nchimbi na IGP Mwema, tuonesheni kwa vitendo uwajibikaji wenuktk kushughulikia kero hizi za amani ya Watanzania.

    ReplyDelete
  4. Msimamo dhabiti wa Rais na serikali yake kwa ujumla dhidi ya vitendo hivi vya mashambulizi dhidi ya imani ya kikristo hapa nchini umekosa ndiyo maana vitendo hivi vinazidi kushamiri siku hadi siku licha ya kauli za rais na serikali zisizo na vitendo.Rais Kikwete achukue changamoto ya mtangulizi wake Benjamini Mkapa kuwa wakati wake dini zilikua zikihubiri amani na hata wakati wa Nyerere hatukuona haya shauri ya misimamo yao dhabiti.Vinginevyo Kikwete ataingia katika historia ya kuiparaganyisha nchi.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad