Na Mwandishi Wetu
KUANZISHWA kwa utaratibu wa Tiba kwa Kadi (TIKA) katika Mkoa wa Dar es Salaam unaosimamiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za matibabu na kupunguza tatizo la ukosefu wa dawa.
Hatua hiyo itafanikiwa kutokana na usimamizi wa huduma hiyo kuwa chini ya Manispaa husika ambayo itakuwa na uwezo wa kutumia fedha zitokanazo na Mfuko huo kununulia dawa na kuboresha mazingira ya vituo ili wananchi wapate huduma bora za matibabu.
Hayo yamejitokeza katika mafunzo ya siku moja kwa Timu ya Uendeshaji ya Huduma za Afya (CHMT) na wakuu wa Idara katika Manispaa ya Temeke ikiwa ni hatua ya uanzishwaji wa Mfuko huo.
Akieleza manufaa ya TIKA kwa wananchi, Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF/TIKA), Rehani Athuman alisema kuwa utaratibu huo utamhakikishia mwananchi kupata matibabu na familia yake kwa mwaka mzima kwa kila mwanakaya aliyechangia.
“Wananchi wanamilikishwa uendeshaji wa Mfuko na huduma za afya kwa ujumla hivyo inawezekana kabisa kujipanga na kutoa huduma bora kwa wanachama wake kwa kuongeza wigo wa mafao kama rufaa,” alisema Athuman.
Alisema kuwa kwa sasa kazi inayofanyika ni kuielimisha jamii dhana na muundo wa TIKA pamoja na faida zake, kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi za manufaa ya mfuko ili wafikie maamuzi sahihi ya kujiunga na kuchangia kwa hiari.
“Fedha zitokanazo na Mfuko huu zinatakiwa kuwekwa kwenye kipaumbele cha ununuzi wa dawa kwa asilimia 67 ili wananchi waone thamani ya fedha wanazochanga na kinachotakiwa kuepukwa ni pamoja na fedha hizo kuelekezwa katika matumizi yasiyohusiana na huduma za matibabu,” alisema Athuman.
Kwa upande wa viongozi hao baada ya kupewa mafunzo hayo, walisema kuwa utaratibu huo ni mzuri na utaweza kuwasaidia wananchi wa Manispaa ya Temeke kwa kuwapunguzia adha wanayokumbana nayo kwa sasa ya kujilipia matibabu kila wanapougua.
Walikubaliana wote kwa pamoja kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika kupambana na changamoto zilizoko katika upatikanaji wa huduma za matibabu ili uanzishwaji wa TIKA ufanikiwe na wananchi wanufaike zaidi.
NHIF iko kwenye mchakato wa kuanzisha Mfuko huo Mkoa wa Dar es Salaam ambapo tayari umeshakutana na Manispaa ya Ilala na Temeke kwa ajili ya mafunzo kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu huo.


No comments:
Post a Comment