HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 9, 2012

NHIF anzisheni TIKA haraka - Madiwani

Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Kheri Kessy akifungua mafunzo ya uanzishaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii (TIKA) yaliyohusisha Kamati ya Mipango na Fedha na Kamati ya Huduma za Jamii.

Na Mwandishi Wetu

MADIWANI wa Manispaa ya Ilala wameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Uongozi wa Manispaa hiyo kuharakisha taratibu za uanzishaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii (TIKA) ili wananchi wawe na uhakika wa matibabu.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Bi. Angelina Malembeka baada ya kumalizika kwa mafunzo ya uanzishaji wa Mfuko huo.

Alisema kuwa mpango huo ni mzuri na unalenga moja moja kwa moja kumsaidia mwananchi hivyo wakiwa kama wawakilishi wa wananchi watalipa kipaumbele jambo hilo hasa baada ya kufika katika ngazi ya kutoa maamuzi.

"Jambo la afya ni suala nyeti sana ambalo tunapaswa kulipa msukumo mkubwa, hivyo NHIF na Watendaji katika Manispaa yetu harakisheni mchakato huu na litakapofika kwetu tutalipa msukumo kwa manufaa ya wananchi wetu," alisema Malembeka.

Awali baadhi ya madiwani walihoji ni kwa namna gani Mfuko huo umejipanga kutoa huduma kwa wanachama watakaojiunga au kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma.

Akijibu maswali yaliyohojiwa, Mkurugenzi wa Uhai wa Mfuko,Bw. Michael Mhando alisema kuwa usimamizi mkubwa wa huduma zitolewazo na mfuko huo ziko kwenye Manispaa husika chini ya Bodi za Huduma za Afya za Manispaa utaratibu utakaowezesha kujipanga na kusimamia vyema ubora wa huduma kwa wanachama.

Suala jingine ambalo lilihojiwa ni wigo wa huduma hiyo kwa wanachama ambapo walitaka kujua kama utaweza kumhudumia mwanachama nje ya nchi, Katika hilo, Bw. Mhando alisema kuwa utaratibu wa kutibu wanachama nje ya nchi haupo kwa sasa na kinachofanywa na NHIF ni kuboresha na kujenga uwezo wa vituo vya kutolea afya vya ndani ili viweze kutoa huduma bora.

Akielezea umuhimu wa Tiba kwa Kadi, Bw. Mhando alisema kuwa utasaidia kutatua changamoto ya upandaji wa gharama za matibabu na kupunguza mzigo wa Manispaa wa kutoa huduma za matibabu kwa makundi maalum.

"Mbali na umuhimu huo, TIKA itasaidia kuongezeka kwa rasilimali fedha katika utoaji wa huduma za Afya ili kukabiliana na changamoto za upatikaji wa dawa na vifaa tiba lakini pia ushirikishaji wa wananchi katika kuchangia huduma za afya na kujiletea maendeleo," alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad