Wajumbe wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa katika mkutano wao ambao haukuwa rasmi, ambapo walipokea taarifa ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Kofi Annan ambaye amepewa jukumu la kushughulia mgogoro unaoendelea nchini Syria. katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amesema serikali ya Syria licha ya kukubali kutekeleza mapendekeo sita yaliyotolewa na mjumbe maalum, bado hali ni tete na damu inaendelea kumwagia. Kwa upande wake kofi Annan aliyezungumza kwa njia ya Video-Link kutokea Geneva anasema wakati umefika kwa pande zote mbili kusitisha mapigano mara moja na kuondoa majeshi yao kwenye maeneo ya watu na kupisha mazungumzo ya kurejesha amani.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Mhe, Kofi Annan akisalimiana na Meja Jenerali Robert Mood raia wa Norway ambaye ni Kiongozi wa Timu ya Ulinzi ya Umoja wa Mataifa itakayokwenda nchini Syria kusimamia uondoaji wa wanajeshi na silaha katika maeneo ya watu.
Na Mwandishi Maalum
New York
Licha ya kwamba serikali ya Syria imekubali kutekeleza mapendekezo ya kumaliza vurugu yaliyotolewa na Mjumbe Maalum wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Kofi Annan. Damu bado inaendelea kumwagika nchini humo
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon wakati Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, lilipokutana siku ya Alhamisi katika mkutano wake usio rasmi ili kupokea taarifa ya maendeleo ya juhudi zinazofanywa na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za Kiarabu, Mhe. Kofi Annan.
Na kwa sababu hiyo Ban Ki Moon ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono na kusaidia juhudi za mjumbe huyo maalum. Huku akilitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuendelea kutoa shinikizo kwa pande zote zinahohusika na mgogoro huo kukomesha vita na mateso.
Mkutano huo uliitishwa na Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Bw Nassir Abdulaziz Al Nasser ambapo Mhe. Kofi Anna alizungumza kwa njia wa Video-Link kutokea Geneva
“ Pamoja na serikali ya Syria kukubali mpango na mapendekezo ya awali ya Mjumbe Maalum ya kutatua mgogoro huo, ghasia na mashambulizi katika maeneo ya raia hayaja simamishwa. Hali katika nchi hiyo inaendelea kuzorota” akasema Ban Ki Moon.
Akawaeleza wajumbe wa UM kwamba Mhe. Annan aliwasilisha mapendekezo Sita wakati alipokuwa Damascus (Syria )mwezi uliopita. Baadhi ya mapendekezo hayo ni kusitisha ghasia na mauaji, kutoa fursa kwa mashirika ya kimataifa kutoa misaada ya kibinadamu, kuachia wafungwa na kuanzisha majadiliano ya kisiasa.
“ Serikali ya Syria ilimtaarifu Mjumbe Maalum kwamba itakuwa imekamilisha kuondoa askari na silaha nzito kutoka katika maeneo ya watu ifikapo April 10 mwezi huu. Mamlaka ya Syria inawajibu sasa wa kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo kwa ukamilifu na bila ya masharti yoyote” akasisitiza Katibu Mkuu.
Akatoa wito kwa Rais wa Syria Bashar al- Assad, serikali yake na wote wanaohusika kuonyesha utashi wa kiuongozi na pia akatoa wito kwa upande wa upinzani nao kuwa tayari kusitisha mapigano na unyanyasaji kama ilivyoanishwa kwenye mpango wa Mhe. Annan.
“ wengi wenu mliopo hapa mmetaka kuwapo kwa juhudi za mwisho za kuutatua mgogoro huu kwa njia za amani. Na baadhi yenu mmeonyesha wasi wasi wenu kwamba vita kamili inaweza kujitokeza ikiwa juhudi za kidiplomasia zitashindwa. Ni kweli hali nchini Syria inaendelea kuzorota. Ninawaomba muunge mkono juhudi za Mhe. Annan katika kipindi hiki kigumu” akasihi Ban Ki Moon.
Aidha Ban Ki Moon amebainisha kwamba matumizi ya kijeshi nchini Syria hayatakuwa na manufaa yoyote na badala yake amesisitiza kuanza kwa mchakato wa mazungumzo na kwamba muda wa maneno umekwisha na jumuia ya kimataifa inaonyeshe kwamba iko pamoja na wananchi wa Syria.
Kwa upande wake Mjumbe Maalum Kofi Annan amesema serikali ya Syria na upande wa wapinzani lazima sasa waache mapigano na vitendo vyote vya unyanyasaji.
Na kuongeza kwamba kama ilivyokubaliwa na mamlaka ya Syria timu ya umoja wa mataifa, ikiwa ni pamoja maofisa kutoka Idara ya Operesheni za Kulinda Amani (DPKO), watakwenda nchini humo ili kuanza maandalizi ya kiufundi kwa ajili ya kupeleka waangalizi wakufuatilia usitishaji wa vita vya kutumia silaha na utekelezaji kamili wa mapendekezo yake sita ya kuleta amani.
“ Naomba makamanda wa serikali na upinzani kutoa maelekezo ya wazi kwa walinzi wa amani wa umoja wa mataifa wakishafika nchi humo kusimamia uondoaji wa majeshi” akasema Annan”
Akasisitiza kwamba serikali ya Syria ilimhakikishia kwamba ifikapo Aprili 10 itakuwa imeondoka vikosi vyake katika makazi ya watu.
“ Baada ya serikali kukamilika kwa zoezi la kuondoka majeshi hapo Aprili 10. Pande zote zitatakiwa kusitisha kabisa mapigano ifikapo saa 0600 kwa saa za Damascus alhamisi, Aprili 12. Akasema Mjumbe Maalum
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 8,000, wengi wao wakiwa raia wameuawa,pamoja na wengine milioni wakihitaji misaada ya kibinadamu ndani ya Syria huku maelefu wengine wakiwa wameyakimbia makazi yao tangu mapigano yalipoanza nchi humo.
Hao wanaoenda syria wawe makini wasije wakawasha moto mpya, mwisho nawapa pole wasanii wote nikiwemo mimi na watanzania kwa ujumla kwa kifo cha Kanumba. Niite Abel Saabuni
ReplyDelete