HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 2, 2012

SAFARI LAGER YATANGAZA KUKAMILIKA KWA NGAZI YA KWANZA YA SHINDANO LA “WEZESHWA NA SAFARI LAGER”

Meneja wa bia ya Safari Lager,Oscar Shelukindo (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kupatikana kwa washindi wa Programe ya Wezeshwa na Safari Lager ambapo jumla ya wajasiria mali 64 wamefaulu kuingia kwenye hatua ya Mwisho.Kushoto ni Mratibu wa programu hiyo Laurence Andrew.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager imetangaza kukamilika kwa ngazi ya kwanza ya kampeni yake ya kuwatafuta na kuwawezesha wajasiriamali wadogowadogo katika shindano la “Wezeshwa na Safari Lager”.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam Meneja wa bia ya Safari Lager Bw. Oscar Shelukindo alisema ngazi ya kwanza ya shindano ilihusisha wajasiriamali wadogowadogo kujaza kwa usahihi na kutuma fomu za maombi ya ruzuku. Jumla ya fomu 9,738 zilikusanywa kuanzia kampeni ilipozinduliwa rasmi November 24 mwaka jana.

 “Tunawashukuru watanzania wote kwani kumekuwa na maombi kutoka mikoa mingi ya Tanzania, jumla ya mikoa 18 imeshiriki. Hii inaonyesha watanzania wana muamko wa kujiendeleza na kuendeleza pia jamii inayowazunguka, hilo ndio lengo kuu la shindano.

Bw. Shelukindo alieleza pia ya kwamba fomu hizi zimechujwa na wataalamu mahiri katika mambo ya biashara. Wamepatikana jumla ya wajasiriamali 80 ambao watatembelewa na majaji ili kukagua biashara zao na 64 watakaofaulu watapatiwa mafunzo maalumu ya wiki moja. Baada ya mafunzo wajasiriamali hawa watakabidhiwa ruzuku zao katika hafla maalum, ruzuku ya vitendea kazi vyenye thamani ya jumla ya shilingi 200,000,000 itakabidhiwa kwa wajasiriamali watakaofaulu.

Akizungumzia ushiriki jaji mkuu Bw. Joseph Migunda wa taasisi ya TAPBDS alisema wajasiriamali wa rika zote wamejitokeza, idadi ya wanaume walioshiriki ni asilimia 65 ya washiriki wote, na wanawake ni asilimia 35. 

Alisema pia maombi yametoka katika fani nyingi sana, mafundi wa aina mbalimbali kama magari, nguo na kuchonga mizinga ya asali, watoa huduma kama hoteli, mitandao na mawasiliano, wazalishaji kama wa vyakula vya kusindika, kukoboa nafaka nk wote wamejitokeza kuomba kuwezeswa na Safari Lager. 

Alisema vigezo vilivyotumika ni mtu awe na biashara yake mwenyewe, mchapakazi na mwenye lengo la kujiendeleza na kusaidia jamii inayomzunguka. Majaji waliangalia ubunifu wa wazo la biashara, uwezo wa kujieleza na kama fomu imejazwa vizuri na ina viambatanishi vyote. Asilimia 18 ya fomu zote hazikujazwa kwa usahihi.

Akielezea hatua inayofuata, Bw. Lawrence Andrew meneja uendeshaji wa kampuni ya Integrated Communications inayoratibu mashindano haya alisema Baada ya mafunzo wajasiriamali watakaofaulu watakabidhiwa ruzuku zao katika hafla zitakazofanyika Dar, Mwanza, Arusha na Mbeya kuanzia mapema mwezi wa nne.

Bwana Shelukindo alimaliza kwa kuwashukuru watanzania wote kwa ushiriki huu, na aliwaomba radhi wajasiriamali ambao wanaendelea kutuma na ambao bado wako na fomu kwamba muda wa kurudisha umekwisha, tunawaomba washiriki tena shindano lijalo la Wezeshwa na Safari Lager.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad