HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 30, 2012

OMBI LA JUMUIYA YA WATANZANIA UGIRIKI KWA NDUGU ZETU WANAOPITIA UBATANI

Wiki iliyopita nilikuwa kwenye ofisi ya Jumuiya yetu nikiongea na baadhi ya vijana waliowasili hivi karibuni kutokea “UBATANI”(Hili ndilo jina tulitumialo badala ya “UTURUKI”kama vile litumikavyo jina “UMANGANI” badala ya “UGIRIKI” )

Ilijionesha wazi katika mazungumzo yetu kuwa picha waliyokuwa wakiidhania ilikuwa ni tofauti mno na hali halisi waliyokumbana nayo.Baadhi yao wamekuja na seaman book wakitegemea wangepata kazi ya melini mara tu watapofika!!!

“Niliambiwa nikifika Umangani kuna meli kibao zinatafuta mabaharia na mshahara ni buku!!!Lakini tangu nimefika hapa nimegundua kuwa zilikuwa ni kamba tu za washkaji maana hata huko bandarini si rahisi kukaribia”Alisema mmoja wa vijana hao kwa unyonge na uchungu.

Mwingine aliongezea akikuna kichwa “Nimelazimika kuomba msaada kwa washkaji zangu waliopo UK ili nitafute mchongo wa kuchomoka maana hali nilivyoiona sivyo nilivyoambiwa na hadi sasa washkaji wenyewe wananipa story tu”

“Mimi rumba nililishtukia tangu pale tulipokuwa tunabinjuka toka ubatani baadae tukakamatwa na kuwekwa kambini,Walipotuachia tuje Athens nikampigia simu mama anitafutie tiketi ya kurudi!!!!Alisema kijana aliyekiri kuwa hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kusafiri nje ya nchi.

Nimelazimika kuielezea mifano hai hiyo nikiwa sina lengo la kufichua siri za jandoni,bali niweze kupata nafasi ya kutoa picha kwa wale wanaopanga kufuata njia hizo hizo bila ya kuwa na picha kamili ya hali halisi itayowakabili ambao wengi wao hawana ule ubavu wa kukabili mazingira kama walivyoyakabili wasafiri wa zamani ambao walivumilia mengi magumu zaidi ya haya.

Namalizia kwa taarifa ifuatayo:

Serikali ya hapa imepitisha bungeni hivi karibuni sheria ya kuanzisha kambi za kuwahifadhi wageni wanaoingia nchini kinyume cha sheria. Kuanzia sasa wageni wakibinjuka hawatakuwa wanaachiwa waende Athens, badala yake watahifadhiwa (WATAFUNGWA) katika kambi hizo hadi pale utapopatikana uwezekano wa kuwarudisha makwao.

Tunawaomba vijana wote wataofikiria kupitia njia hizi walijue hili, ili wasije wakawatia presha wazazi wao pindi watapokuwa wamefungwa na hatimae kurudishwa.

Niliyoyasema si vitisho bali ni wajibu wetu kuwajuza ndugu zetu wa nyumbani wasioijua hali halisi ya huku na baada ya hapa wao wana haki ya kuamua kuja au kutokuja. .

Kwa kuhakiki maelezo niliyoyatoa kuhusu kambi za kuwafungia wageni wanaweza kuingia google kabla hawajaamua kuja.TAARIFA YA MWISHO NI KUWA WAMEPELEKWA WAGENI 56 KATIKA KAMBI MPYA ILIYOPO KIJIJI CHA AMYGDALEAS.ITAYOKUSANYA WAGENI 1,200.

Ahsanteni

KAYU LIGOPORA

KATIBU MKUU JUMUIYA YA WATANZANIA UGIRIKI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad