HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, February 4, 2012

Dkt. Mukangara atoa rai kwa wabunge kuanzisha vikundi mbalimbali vya mazoezi na michezo kwenye majimbo yao

Na Lydia Churi, MAELEZO, Dodoma

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameombwa kuanzisha vikundi mbalimbali vya mazoezi na michezo kwenye majimbo yao ili kusaidia kutoa ajira kwa vijana na kuwalinda vijana wasijiingize kwenye vitendo viovu katika jamii.

Rai hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara alipokuwa akifungua mazoezi ya viungo kwa waheshimiwa wabunge na wananchi yaliyoendeshwa na kikundi kijulikanacho kwa jina la (Kitambi Noma) kutoka Unguja yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Dkt. Mukangara alisema serikali inatambua umuhimu wa kufanya mazoezi hivyo aliwaomba waheshimiwa wabunge kuanzisha vikundi kwenye majimbo yao hasa mashuleni vitakavyowasaidia watoto kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi.

Aliahidi kuwa wizara yake itaendelea kuunga mkono watanzania wote wanaojishughulisha na michezo katika jamii na itaendelea kuweka mikakati endelevu ya kuhakikisha michezo inaboreshwa nchini.

Alisema mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara yatawasaidia vijana kushinda katika mashindano mbalimbali pindi yanapotokea kwa kuwa watakuwa na ubunifu na afya zao zitakuwa zimeimarika.

Naibu waziri huyo aliwataka waheshimiwa wabunge kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kushiriki katika michezo kwa kuwa itawasaidia kuimarisha afya zao na kuepukana na magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine yanayosababishwa na ongezeko la uzito kupita kiasi.

Aliwaomba waheshimiwa wabunge kuwahimiza wananchi kwenye majimbo yao kufanya mazoezi na kushiriki katika michezo kwani michezo ni afya, hujenga mshikamano, amani, upendo, nidhamu na utamaduni wa ushindani.

Klabu ya michezo na mazoezi ya viungo ya ‘Kitambi Noma’ ambayo mlezi wake ni Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa ilianzishwa kwa madhumuni ya kuboresaha afya za wanakikundi na kutoa ujumbe kwa watanzania kuwa mazoezi ya viungo ni muhimu kwa afya ya binadamu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad