HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 25, 2012

Wabunge wa Kamati ya Huduma za Jamii wafanya ziara jijini Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Ndungulile akisikiliza kero za wananchi waliofika kwenye kituo cha afya cha Sangabuye kilichopo wilayani Ilemela baada ya kutembelea kituo hicho na wajumbe wa kamati yake.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD nchini Bw. Joseph Mgaya akielezea mafanikio na changamoto zinazowakabili katika MSD ambapo aliweza kuelezea jinsi wanavyoidai serikali fedha nyingi. wengine anayemfuata ni Mwenyekiti wa bodi ya MSD Bi Eva Nzaro, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Ndungulile, na Mjumbe wa bodi ya MSD Bi Tecla Shangali.
Mbunge wa Nzega (CCM) Dkt Hamisi Kigwangwalah (wa kwanza kulia) akichangia suala la serikali kudaiwa fedha nyingi na MSD kiasi cha zaidi shilingi bilioni 45.6 wakati kamati hiyo ilipotembelea ghala la bohari kuu kanda ya ziwa mjini Mwanza.
Wabunge wa Kamati ya Huduma za Jamii wakiwa pamoja na Makamu Mwenyekiti wao Dkt Ndugulile, wakimsikiliza Mkurugenzi wa kanda ya ziwa wa MSD akitoa maelezo namna wanavyoweza kuhifadhi dawa kisha kuzisambaza kwa wateja wao mbalimbali wa mikoa ya Mwanza, Musoma, Bukoba, Shinyanga na mkoa mpya wa Geita.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Faustin Ndungulile (aliyevaa shati la kitenge karibu na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Eng. Evarist Ndikilo, wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa mkoa huyo wakijitambulisha kuhusu kufanya ziara ya siku tatu mkoani humo kutembelea sekta ya afya.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sangabuye Dkt Charles Chacha (mwenye shati la kitenge aliyenyanyua mikono) akiwaeleza wajumbe wa kamati ya huduma za jamii waliofika katika kituo hicho ambapo mganga huyo mfawidhi alieleza kwamba kituo hicho kinakimbiwa na madaktari kutokana na kuwepo kwa sababu za ushirikina ambapo unapolala usiku watu wanafika katika nyumba yako na kukutoa nje.
Pamoja na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Eng. Ndikilo kulalamika kwamba kuna uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali nyingi mkoani humo licha ya MSD kuwasilishiwa fedha lakini wajumbe wa kamati hiyo walishuhudia shehena na mabox ya dawa yakiwa yamehifadhiwa kwenye bohari hiyo ya madawa kanda ya ziwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari Kuu ya Madawa nchini (MSD) Bi Eva Nzaro (wa kwanza kulia) akiwa na mgeni wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Dkt Ndungulile (mwenye shati la kitenge) akimuongoza pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo kwenda kutembelea bohari ya kuhifadhia dawa ya Kanda ya Ziwa iliyopo Jijini Mwanza.

Na Mashaka Mhando,Mwanza

WABUNGE wa Kamati ya Huduma za Jamii, wameitaka serikali kulipa deni la shilingi bilioni 45.6 wanazodaiwa na Bohari Kuu ya taifa ya Madawa nchini (MSD), ili waweze kukabili changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kuagiza dawa nje na kuzisambaza katika hospitali kwa wakati.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea bohari Kuu ya taifa ya madawa ya Kanda ya Ziwa, wabunge hao wamesema kuwa MSD imekuwa ikinyooshewa vidole ya ukosefu wa madawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali hapa nchini, lakini bohari hiyo imekuwa ikishindwa kuagiza dawa nje ya nchi kutokana na kukosa uwezo wa kifedha kuagiza dawa hizo na kusababisha kero katika maeneo hayo.

Mbunge wa Nzega (CCM) Dkt Hamisi Kigwangwalah alisema endapo serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, itashindwa kulipa deni hilo hadi kufikia Juni mwaka huu, hawatapitisha bajeti ya Wizara hiyo kutokana na kusababisha matatizo katika sekta ya afya nchini kwa kuwapa tabu wananchi ambao baadhi yao wamekuwa wakitoa michango katika mifuko ya afya ya jamii.

"Tatizo la ukosefu madawa katika hospitali zetu silo la MSD hata kidogo, tatizo hapa ni Wizara ya afya wananchi wamekuwa na matatizo mengi ya ukosefu wa madawa katika vituo vyetu vya afya na zahanati, kama serikali itashindwa kutatua matatizo ya msingi katika huduma za afya hayo malengo ya milenia tuliyoyaweka tutayafikia vipi, sasa tutaweka azimio leo hii kama serikali haitalipa basi hatutapitisha bajeti ya wizara ya afya, katika bunge la bajeti linalokuja" alisema Dkt Kigwangalah.

Mbunge wa Ilemela Chadema, Bw. Hyness Kiwia akichangia suala hilo alisema kuwa haamini kama MSD wamekuwa wakipata vikwazo vya kushindwa kuagiza na kusambaza dawa katika hospitali za hapa nchini akawataka waandae taarifa ambayo watakiri kwamba kutokana na serikali kushindwa kulipa deni la fedha hizo ndiyo sababu wanashindwa kusambaza dawa badala ya kukopwa dawa kila mwaka na wizara hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Joseph Mgaya alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na deni wanalolidai serikali ya kiasi hicho cha fedha na kwamba mwaka jana waliiomba serikali iwalipe kiasi cha shilingi bilioni 7 ili wawasilishe manunuzi nje kwa ajili ya kusambaza dawa hapa nchini lakini serikali haikuwa na fedha badala yake ikasema katika hospitali hakuna dawa wakakopa madawa yenye thamani ya shilingi bilioni 3.

Awali wakipata maelezo ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Evarist Ndikilo, alisema MSD wamekuwa wakishindwa kuwasilisha madawa katika hospitali mbalimbali zilizopo mkoani humo licha ya kupatiwa fedha za vituo hivyo hatau ambayo alisema ni bora sasa serikali kupitia wabunge hao wakatunga sheria ambayo itawaruhusu watu wengine kusambaza dawa badala ya MSD ili kuondoa usumbufu wa kukosa dawa mara kwa mara.

"Dawa MSD hakuna lakini fedha zao zipo kule jambo ambalolinasababisha washindwe kununua dawa mahali pengine kutoka na sera zilizopo MSD pekee wenye jukumu la kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa," alisema Injinia Ndikilo na kuongeza MSD wanatakiwa kununua dawa kwa uharaka na hospitali waruhusiwe kunua dawa mahali pengine.

Akizungumza katika majumuisho Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Faustin Ndungulile aliitaka MSD kuhakikisha inanunua kila wakati dawa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kwa mahitaji mengi katika zahanati na vituo vya afya kutokana na fedha ambazo wanakuwa nazo kuliko kusubii dawa hizo ziishe katika maeneo hayo ikiwemo kutaza upya suala la manunuzi ya madawa nje ya nchi.

Alisema ni vema viwanda vya dawa vilivyopo hapa nchini vikaimarishwa na MSD wakatoa kipaumbele katika kununua dawa katika viwanda hivyo kuliko kupeleka fedha nje ambako kumekuwa hakuleti nafuu kwa hospitali nyingi hatua ambayo ametaka viwanda hivyo vijengewe uwezo ili hatimaye viweze kutosheleza soko la dawa hapa nchini.

Kuhusu deni hilo wanazodaiwa serikali na MSD alisema serikali ijitahidi kulipa kadri inavyopata fedha ili kuondoa uwezekano wa mizozo isiyokuwa na sababu kwa wabunge wa kamati hiyo katika bunge lka bajeti lijalo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad